Na Emmanuel Chibasa
Katika kijiji cha Bugwema,
Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, Briton Moris anatumia pampu ya mafuta kumwagilia
shamba lake la mahindi lenye ukubwa wa ekari tatu. Hata hivyo gharama za mafuta
anazotumia katika shughuli hiyo zimekuwa changamoto kubwa, kiasi cha kuathiri
uwezo wake wa kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa kiwango anachokihitaji.
Anasema ili kumwagilia ekari
moja, hutumia takribani lita 20 za mafuta kwa siku, hali inayoongeza gharama za
uzalishaji, hasa kutokana na aina ya ardhi ya eneo analolima ambayo anasema
inahitaji maji mengi.
“Kwa siku natumia lita 20
kumwagilia ekari moja kutokana na ardhi kuwa ni mbuga ambayo inahitaji
umwagiliaji maji mengi kwa sababu ardhi ni tepe tepe,” anasema Briton.
Changamoto kama hiyo
inawakabili wakulima wengine katika maeneo ya vijijini mkoani Mara, ambako
kilimo kinaendelea kutegemea kwa kiasi kikubwa mvua. Kutotabirika kwa misimu ya
mvua na vipindi vya ukame kunawafanya baadhi ya wakulima kutafuta njia mbadala
za kuhakikisha wanaendelea kuzalisha chakula na kupata kipato.
Hata hivyo, kutumia pampu za
mafuta katika kilimo cha umwagiliaji kunahitaji fedha za kununua mafuta na
kugharamia uendeshaji. Kwa wakulima wadogo ambao kipato chao hutegemea mavuno,
gharama hizo zinaweza kupunguza faida au kuwafanya washindwe kupanua mashamba
yao.
Joseph Omenya, mkulima wa
bustani katika kijiji cha Bugwema, anasema hata katika eneo dogo analolima
nyanya na mboga mboga, matumizi ya mafuta ni sehemu ya gharama anazopaswa
kuzikabili ili kuendelea kumwagilia mazao yake.
“Hili shamba dogo la bustani
unaloliona kwa wiki natumia lita saba, ndani ya siku tatu natumia lita tatu na
nusu kulingana na ardhi tunayotumia hapa katika shughuli zetu za kilimo,”
anasema Joseph.
Kwa wakulima wanaotegemea
bustani kama chanzo cha chakula na kipato, gharama za umwagiliaji zinaweza
kuathiri uwezo wao wa kuendeleza uzalishaji na kuendesha shughuli za kilimo
zisizo na tija. Hali hiyo inaonyesha kuwa changamoto ya nishati haiwahusu
wakulima wenye mashamba makubwa pekee, bali pia wale wanaolima maeneo madogo.
Loyce Joshua, mkulima wa
mboga mboga anasema pia hutumia mafuta katika kuendesha pampu ya kumwagilia
shamba lake. Anaeleza kuwa licha ya kutumia fedha katika umwagiliaji, bado
hajaona mafanikio anayoyatarajia, huku akiamini kuwa matumizi ya teknolojia ya
sola yanaweza kuwa mbadala wa kumsaidia kupunguza gharama.
Kwa upande mwingine, Penina
Elisha anasema ameshindwa kupanua shughuli zake za kilimo kutokana na
changamoto ya kupata maji. Kwa sasa hulazimika kuchota maji kwa mikono kwa
sababu chanzo cha maji hakipo karibu na shamba lake.
“Mimi hapa nalima shamba
kidogo sababu nasomba maji kwa mikono na maji hayapo jirani na shamba, lakini
endapo nitawezeshwa na serikali kwa kupata miundombinu ya sola kwa ajili ya
kumwagilia nitaweza kulima shamba kubwa na kupata faida,” anasema Penina.
Ushuhuda wa wakulima hawa
unaonyesha kuwa changamoto za umwagiliaji zinatofautiana kulingana na ukubwa wa
shamba, aina ya mazao, upatikanaji wa maji na uwezo wa kifedha. Hata hivyo,
wote wanakutana na suala moja muhimu: gharama na ugumu wa kupata maji kwa ajili
ya kuendeleza uzalishaji.
Teknolojia ya sola kama mbadala wa gharama za
mafuta
Katika mazingira hayo teknolojia ya pampu za umwagiliaji zinazotumia
nishati ya jua na zinazoweza kuhamishwa kutoka shamba moja kwenda jingine
inaibua fursa kwa wakulima wadogo. Tofauti na baadhi ya mifumo ya sola
inayofungwa katika eneo moja, teknolojia hii inawezesha pampu na paneli za sola
kusafirishwa na kutumiwa katika maeneo tofauti kulingana na mahitaji.
Elizabeth Komanyani, mtaalamu
wa nishati ya umeme jua ambaye pia ni afisa masoko wa kampuni ya Simu Solar
Tanzania, anasema pampu za sola zinaweza kusaidia wakulima kupunguza utegemezi
wa mafuta katika shughuli za umwagiliaji.
Anasema teknolojia hiyo
inaweza kuwa na manufaa kwa wakulima wadogo kwa sababu haihitaji ununuzi wa
mafuta kila siku kama ilivyo kwa pampu zinazotumia petroli.
“Solar pump ni uwekezaji wa mara moja, na mkulima anaweza kuzihamisha kwa urahisi kutoka shamba moja hadi jingine. Matumizi ya teknolojia hii yanaweza kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kutokomeza umaskini,” anasema Elizabeth.
Hata hivyo, anasisitiza
umuhimu wa wakulima kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kununua vifaa hivyo.
Anasema wataalamu wanapaswa kutembelea mashamba na kutathmini vyanzo vya maji
ili kubaini aina ya pampu inayofaa kulingana na mazingira ya eneo husika.
“Wakulima wa kilimo cha
umwagiliaji kabla ya kununua vifaa vya sola wanapaswa kuwaona wataalamu ili
kutembelea maeneo yao, kuangalia vyanzo vya maji na kushauri pampu zinazotakiwa
kutumika,” anasema.
Elizabeth anaeleza kuwa kuna
mifumo tofauti ya pampu za sola kulingana na chanzo cha maji. Baadhi hutumika
katika maji ya visima, huku mingine ikifaa kwa vyanzo kama maziwa, mabwawa na
mito.
“Kuna aina mbili za solar kwa
ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kuna pampu zinazotumika katika maji ya visima,
lakini pia kuna pampu ambazo vyanzo vyake vya maji ni ziwa, mabwawa au mito.”
Anasema
Ushauri huo unaonyesha kuwa
si kila pampu inafaa kwa kila shamba. Mkulima anahitaji kufahamu kina cha maji,
umbali wa chanzo, mwinuko na mahitaji ya maji ya zao analolima kabla ya kuamua
kununua mfumo fulani.
Pampu zinazohamishika zinafanyaje kazi?
Mhandisi Adrian Edwin
Mapunda, mtaalamu wa nishati ya jua kutoka ELICO Foundation, anasema taasisi
hiyo imekuwa ikisaidia wakulima katika miradi ya umwagiliaji na kuendeleza
mifumo ya nishati ya jua inayohamishika pamoja na mifumo midogo ya umeme
inayohusiana na shughuli za kilimo vijijini.
Kwa mujibu wa maelezo ya
kiufundi yaliyotolewa na ELICO Foundation, mfumo wao wa pampu za maji una uwezo
wa kati ya nguvu farasi 0.5 na 2 (HP), ukiendeshwa na paneli za sola zenye
uwezo wa wati 600 hadi 1,200 zilizowekwa kwenye toroli maalumu.
Taarifa za mfumo huo zinaeleza kuwa, kutegemea usanidi wa vifaa na mazingira ya matumizi, pampu inaweza kusukuma hadi lita 20,000 za maji kwa siku na kuyafikisha umbali wa hadi kilomita 0.8.
Uwezo huo unaonyesha namna
teknolojia ya sola inayohamishika inavyoweza kutumiwa na wakulima wanaohitaji
kusafirisha maji kutoka chanzo kilichopo mbali na mashamba yao. Hata hivyo,
kiwango halisi cha maji kinachoweza kusukumwa kinaweza kutofautiana kulingana
na umbali, mwinuko, aina ya pampu na hali ya mfumo.
Mapunda anasema teknolojia
hiyo inalenga kuwapatia wakulima wadogo mbadala wa pampu zinazotumia petroli,
ambazo kwa maelezo yake zinahitaji gharama za uendeshaji na matengenezo.
“Kwa kubadilisha pampu za
mafuta ya petroli ambazo ni ghali na zinahitaji matengenezo mengi, mifumo ya
umwagiliaji ya jua ya ELICO inatoa mbadala wa kimsingi na wenye ufanisi
unaolingana na mahitaji ya wakulima wadogo,” anasema Mapunda.
Anaeleza kuwa pampu hizo
zinaweza kuhamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine kwa kutumia toroli
lililowekwa paneli za sola. Hivyo, wakulima wanaweza kutumia mfumo huo katika
maeneo tofauti badala ya kuufunga sehemu moja tu.
Kwa mujibu wa Mapunda, mifumo
ya usambazaji inayotumika na ELICO inajumuisha umiliki, upangishaji na utoaji
wa huduma za umwagiliaji. Njia hizo zinalenga kuwapa wakulima fursa ya kupata
huduma kulingana na uwezo na mahitaji yao.
Uelewa mdogo na fursa ya matumizi ya pamoja
Pamoja na uwepo wa teknolojia
hiyo, uelewa wa baadhi ya wakulima kuhusu uwezekano wa kutumia pampu za sola
zinazohamishika bado ni changamoto.
Chacha Mang’era, mkulima
kutoka Musoma, anasema hakuwahi kufahamu kuwa mifumo ya umwagiliaji inayotumia
nishati ya jua inaweza kuhamishwa kutoka shamba moja kwenda jingine.
“Nilikuwa sijasikia kuhusu
hili kabla na nilidhani umwagiliaji wa kutumia sola unahitaji vifaa vya kudumu
vinavyofungwa sehemu moja, hususan juu ya bati. Sikujua kuwa kuna njia ya
kubeba vifaa hivyo kutoka shamba moja hadi lingine,” anasema Chacha.
Kauli yake inaonyesha umuhimu
wa elimu kwa wakulima kuhusu teknolojia zinazopatikana na namna zinavyoweza
kutumika kulingana na mazingira yao.
Kwa upande mwingine, Mwasi
Zebedayo, mkazi wa Musoma, anaona kuwa uwezo wa kuhamisha pampu hizo unaweza
kuwa na manufaa kwa wakulima wanaomiliki au kutumia mashamba katika maeneo
tofauti. Anasema teknolojia hiyo inaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa mafuta
na kufanya matumizi ya pampu katika maeneo mbalimbali kuwa rahisi zaidi.
Hata hivyo, faida hizo
zinahitaji kutazamwa kwa kuzingatia gharama za awali za kununua vifaa,
matengenezo ya mfumo wa sola na upatikanaji wa wataalamu wa kuuhudumia.
Francis Mtayomba, mkulima
kutoka Rusoli, Musoma Vijijini, anasema wakulima wanaojipanga katika vikundi
wanapaswa kupewa elimu kuhusu teknolojia hiyo ili waweze kuchunguza uwezekano
wa kushirikiana katika ununuzi na matumizi yake.
“Sikujua kwamba tungeweza
kutumia pampu hizi kwa kuhamisha na kutumia kwa pamoja. Tukijipanga na kupata
uelewa zaidi, vikundi vyetu vinaweza kushirikiana kununua na kutumia pampu
hizi, hivyo kusaidia kumwagilia mashamba ya wanakikundi wote kwa pamoja na
kuongeza uzalishaji,” anasema Francis.
Pendekezo hilo linaibua fursa
ya umiliki wa pamoja wa vifaa vya umwagiliaji. Badala ya kila mkulima kununua
mfumo wake, vikundi vinaweza kuchunguza utaratibu wa kumiliki kifaa kwa pamoja,
kukipangisha au kupanga ratiba ya matumizi kwa wanachama.
Mfumo huo unaweza kusaidia
kugawana gharama za ununuzi na matengenezo. Hata hivyo, unahitaji makubaliano
ya wazi kuhusu ratiba za matumizi, uwajibikaji na gharama za uendeshaji ili
kuhakikisha kila mwanachama ananufaika.
Nishati safi na kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi
Sekta ya kilimo ni miongoni
mwa sekta zinazohisi athari za mabadiliko ya tabianchi kwa sababu uzalishaji wa
mazao hutegemea kwa kiwango kikubwa hali ya hewa na upatikanaji wa maji.
Mvua zinapochelewa, kunakuwa
na vipindi virefu vya ukame au misimu inapobadilika, wakulima wanaweza
kukabiliwa na changamoto za kupanga shughuli zao za uzalishaji. Kwa hiyo,
kuongeza uwezo wa kutumia maji kwa ufanisi na kuwa na mifumo mbadala ya
umwagiliaji ni sehemu ya mikakati inayoweza kusaidia kukabiliana na hali hiyo.
Matumizi ya pampu zinazotumia
nishati ya jua yana faida ya kutumia chanzo cha nishati kinachoweza kurejeshwa
badala ya kutegemea moja kwa moja mafuta ya petroli katika uendeshaji wa pampu.
Hii inaweza kusaidia kupunguza matumizi ya mafuta na hewa chafu inayotokana na
uendeshaji wa pampu hizo.
Kwa wakulima kama Briton na
Joseph, ambao tayari wanatumia fedha kununua mafuta, teknolojia hiyo inaweza
kuwa fursa ya kutathmini njia mbadala za kuendesha shughuli zao. Kwa Loyce na
Penina, ambao wameeleza changamoto za gharama na upatikanaji wa maji,
upatikanaji wa mifumo inayofaa unaweza kusaidia kupanua chaguo zao za
uzalishaji.
Pamoja na hayo, teknolojia
hiyo haipaswi kutazamwa kama suluhisho la kila changamoto ya tabianchi. Pampu
haiwezi kutengeneza maji pale chanzo kinapokauka, wala haiwezi kuhakikisha
uzalishaji unaongezeka bila kuzingatia ubora wa udongo, aina ya mazao,
upatikanaji wa pembejeo na usimamizi wa maji.
Kwa maeneo yanayotegemea
vyanzo vya maji kama Ziwa Victoria, ni muhimu kuhakikisha kuwa matumizi ya maji
kwa ajili ya kilimo yanafanyika kwa uangalifu na kwa kuzingatia taratibu za
usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira.
Kwa hiyo, teknolojia ya
umwagiliaji wa sola inapaswa kuunganishwa na elimu ya kilimo himilivu kwa
tabianchi, matumizi bora ya maji, utunzaji wa udongo na mbinu za kuhifadhi
mazao baada ya mavuno.
Gharama, matengenezo na upatikanaji wa huduma
Pamoja na manufaa yanayoweza
kupatikana, changamoto mojawapo ni gharama ya awali ya kununua na kufunga mfumo
wa umwagiliaji wa sola. Kwa wakulima wengi wadogo, gharama hiyo inaweza kuwa
kubwa ikilinganishwa na uwezo wao wa kifedha.
Hali hii inaonyesha umuhimu
wa kuwepo kwa mifumo ya kifedha inayozingatia mazingira halisi ya wakulima.
Taasisi za fedha na wadau wa maendeleo wanaweza kuchunguza mikopo inayolipwa
kwa awamu, huduma za kukodisha vifaa na mifumo ya umiliki wa pamoja ili kupanua
upatikanaji wa teknolojia hiyo.
Pia, mafunzo ya matumizi na
utunzaji wa vifaa ni muhimu. Wakulima wanahitaji kufahamu namna ya kutumia
pampu kwa usalama, kutunza paneli za sola na kutambua hitilafu zinazoweza
kujitokeza.
Upatikanaji wa wataalamu wa
matengenezo karibu na maeneo ya wakulima ni suala jingine la kuzingatia. Vifaa
vinapoharibika na huduma za mafundi hazipatikani kwa wakati, shughuli za
umwagiliaji zinaweza kusimama na kuathiri uzalishaji.
Serikali za mitaa zinaweza
kushirikiana na wataalamu wa kilimo na nishati kutoa elimu kwa vikundi vya
wakulima, kutathmini maeneo yanayofaa kwa matumizi ya teknolojia hiyo na
kusaidia kuweka mifumo ya usimamizi wa pamoja.
Uhifadhi wa mazao na usalama wa chakula
Changamoto za kilimo
haziishii katika uzalishaji pekee. Baada ya mavuno, wakulima pia wanahitaji
mbinu bora za kuhifadhi mazao ili kupunguza upotevu na kuhakikisha wanapata
kipato kinachostahili.
Matumizi ya nishati ya jua
katika kilimo yanaweza kuhusisha zaidi ya umwagiliaji. Teknolojia nyingine,
kama mifumo ya kukaushia na kuhifadhi mazao kwa kutumia nishati safi, inaweza
kusaidia kupunguza upotevu baada ya kuvuna.
Hata hivyo, mifumo ya
umwagiliaji na uhifadhi wa mazao ni suluhisho mbili tofauti zinazohitaji
mipango na vifaa vinavyolingana na aina ya zao na mahitaji ya wakulima.
Kuunganisha hatua za uzalishaji na uhifadhi kunaweza kusaidia kujenga mfumo wa
kilimo unaozingatia usalama wa chakula, kipato cha wakulima na matumizi
endelevu ya rasilimali.
Kwa wakulima wa Musoma na
maeneo mengine ya Mara, teknolojia ya pampu za umwagiliaji zinazotumia nishati
ya jua na zinazohamishika inaibua fursa ya kutafuta njia mbadala za kupunguza
gharama za nishati na kukabiliana na changamoto za mvua zisizotabirika.
Hata hivyo, fursa hiyo
haiwezi kufikiwa kwa kusambaza vifaa pekee. Inahitaji elimu ya kutosha, mifumo
ya kifedha inayowafikia wakulima wadogo, huduma za matengenezo na usimamizi
mzuri wa vyanzo vya maji.
Serikali, taasisi za fedha,
kampuni za nishati safi na mashirika yanayofanya kazi katika sekta ya kilimo
yanapaswa kushirikiana kuhakikisha teknolojia hizi zinafika kwa wakulima wa
vijijini kwa gharama wanazoweza kumudu.
Kwa upande wa wakulima,
vikundi vinaweza kuanza kwa kujifunza kuhusu teknolojia hiyo, kutathmini
mahitaji yao ya maji na kuchunguza uwezekano wa kushirikiana katika matumizi ya
vifaa.
Katika kipindi ambacho
mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuleta changamoto kwa uzalishaji wa
chakula, kuongeza upatikanaji wa teknolojia za nishati safi ni hatua mojawapo
inayoweza kusaidia kujenga kilimo chenye uwezo wa kustahimili mabadiliko hayo.
Kwa wakulima wadogo wa Mara,
pampu ya sola inayoweza kuhamishwa inaweza kuwa zaidi ya kifaa cha kusukuma
maji; inaweza kuwa sehemu ya mjadala mpana kuhusu namna ya kufanya kilimo kiwe
na gharama nafuu, endelevu na kinachoweza kuhimili misimu isiyotabirika.














