Wabunge Mkoa wa Mara wapokea msaada wa mifuko ya Saruji toka Nyansaho Foundation

0


 GHATI MSAMBA, Musoma.

Mkurugenzi wa Nyansaho Foundation na Waziri wa Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Rhimo Nyansaho, ametoa msaada wa mifuko 5,500 ya saruji kwa wabunge wa Mkoa wa Mara kwa lengo la kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Zoezi hilo la ugawaji lilifanyika Machi 22, mwaka huu, katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mara, likihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Nyansaho alisema kuwa lengo la msaada huo ni kuchochea maendeleo ya wananchi kwa kutatua changamoto zilizopo katika sekta muhimu kama elimu na afya, sambamba na utekelezaji wa ilani ya chama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Mhongo, alimshukuru Dk. Nyansaho kwa msaada huo akieleza kuwa utasaidia kuboresha miundombinu ya shule mbili za sekondari kwa mifuko 50, shule saba za msingi kwa mifuko 350 pamoja na zahanati mbili zitakazonufaika na mifuko 100 ya saruji.

Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji, alitoa shukrani zake za dhati kwa kupokea mifuko 500 ya saruji ambayo alisema itasaidia kukarabati shule chakavu na kuboresha mazingira ya kujifunzia ili yaendane na hadhi ya mji.

Aidha, Mgore alieleza kuwa changamoto kubwa katika jimbo lake ni uchakavu wa miundombinu ya shule, na kuahidi kuchangia vifaa vingine ikiwemo mawe, mchanga pamoja na gharama za ufundi ili kuhakikisha ukarabati unafanyika kwa ufanisi.

“Changamoto kubwa iliyopo hapa jimbo la mjini ni uchakavu wa shule, Saruji hizi zitasaidia kukarabati majengo hayo, Mimi nitachangia mawe, mchanga na gharama za ufundi ili kuhakikisha shule zote zinakarabatiwa,” alisema Mgore.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Mathew, alimpongeza Dk. Nyansaho akimtaja kuwa ni kiunganishi muhimu kinachowaleta pamoja wabunge wa mkoa huo na kuwawezesha kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Aliongeza kuwa Dk. Nyansaho amekuwa mstari wa mbele kuchochea maendeleo si tu Mkoa wa Mara bali pia katika maeneo mengine nchini, ikiwemo kutoa misaada katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere pamoja na kutoa ushauri wa kufufua viwanda.

Mbunge huyo pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Dk. Nyansaho katika nafasi yake, akieleza kuwa ni chaguo sahihi linaloleta tija kwa taifa. 

Aidha, alimuomba Dk. Nyansaho aendelee kusaidia jamii, hususan katika Taasisi za dini na kuwawezesha wanawake.

Kwa ujumla, msaada huo unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo katika Mkoa wa Mara kwa kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha ustawi wa wananchi.






Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top