TAKUKURU Kagera yashinda kesi 45 za rushwa, Yarejesha shilingi milioni 277.8

0

 


Na Angela Sebastian 

Bukoba  : TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imeshinda kesi 45 kati ya 50 zilizofikishwa katika mahakama mbalimbali mkoani humo, sawa na asilimia 100, huku ikifanikiwa kurejesha jumla ya Sh. milioni 277.8 zilizokuwa zimetumika kinyume na taratibu katika taasisi mbalimbali.

Katika kipindi cha Aprili hadi Septemba, TAKUKURU imefanikiwa kupata ushindi katika kesi hizo 45, huku kesi tano zikiendelea kusikilizwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Hajinas Onesphory, amesema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kupambana na vitendo vya rushwa na kurejesha fedha za umma.

Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni kurejeshwa kwa Sh. milioni 100 katika akaunti ya Mkurugenzi wa TAKUKURU na kampuni ya STC Construction, fedha zilizohusishwa na ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji katika Kijiji cha Katare, Wilaya ya Bukoba Vijijini.

Aidha, amesema TAKUKURU ilifanikiwa kurejesha Sh. milioni 25.8 zilizokuwa zimejipatia kwa manufaa binafsi mtumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kyerwa pamoja na mzabuni, fedha ambazo awali zilikuwa zimelipwa kwa mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi wa umeme.

Katika hatua nyingine, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kurejesha Sh. milioni 26.1 zilizokuwa ni malipo ya wakulima wa kahawa wa Kyamulaile AMCOS, ambazo zilikuwa zimetumiwa kwa manufaa binafsi na Katibu wa chama hicho, kurejeshwa kwa Sh. milioni 59.2 katika Chama cha Ushirika wa Kahawa Wilaya ya Ngara, Sh. milioni 15 katika akaunti ya Kijiji cha Rwinyana, Sh. milioni 5.5 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara na Sh. milioni 26.6 katika akaunti ya Manispaa ya Bukoba.

Fedha nyingine zilizorejeshwa ni Sh. milioni 5.3 katika akaunti ya Omkishanda AMCOS pamoja na Sh. milioni 5.2 katika akaunti ya Wavuke, Kata ya Nkwenda, Wilaya ya Kyerwa.

Katika kuzuia vitendo vya rushwa, Onesphory amesema TAKUKURU Mkoa wa Kagera pia imefuatilia matumizi ya Sh. bilioni 8.9 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 67 ya maendeleo mkoani humo.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilipokea jumla ya taarifa 252 kutoka kwa wananchi na vyanzo mbalimbali, ambapo taarifa 131 kati ya hizo zilihusu tuhuma za vitendo vya rushwa.





Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top