Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Kagera kwa kipindi cha miezi mitatu Januari hadi Machi mwaka huu wamevuka lengo la ukusanyaji mapato na kukusanya shilingi bilioni 55.
Meneja wa TRA mkoa wa Kagera CPA Joseph Mutalemwa ametoa takwimu hizo Mei 26,2026 katika maonyesho ya elimu ya juu kupitia bodi ya mikopo (HESLB) yanayoendelea katika viwanja vya soko kuu mjini Bukoba.
Amesema kuwa, Mamlaka hiyo katika kipindi cha miezi mitatu Januari hadi Machi mwaka huu walipanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 51 lakini wamevuka lengo hilo na kukusanya shilingi bilioni 55.
Ameeleza kuwa, kupanda kwa lengo hilo kumetokana na elimu ambayo wamekuwa wakitoa maeneo mbalimbali mkoani humo ambayo imesaidia wafanyabiashara kulipa kodi yao bila shuruti.
Mutalemwa amewashauri wafanyabiashara kuwasirisha ritani zao kwa maana ya hesabu za biashara ili kuangalia kiasi cha kodi wanachokilipa kwa mwaka husika kama kinalingana na kiasi cha kodi wanachopaswa kulipa.
“Sheria imeweka uhuru kwamba kabla ya siku 15 muda kuisha mlipa kodi anaweza kuomba muda wa ziada ili awasilishe baadaye taarifa zake za mizania, lakini kuruhusiwa kulipa kwake baadaye hakuondoi wajibu wake wa kulipa kile kiasi cha kodi ambacho anastahili kulipa” amesema CPA Mutalemwa
Baadhi ya wananchi waliofika katika banda la TRA kupata elimu wametaja changamoto ambayo imekuwa ikiwakumba kuwa ni kuwepo vishoka ambao huwatakisha fedha kwa huduma ambazo siyo za kulipia.
Mmoja wa wananchi aliyefika katika banda la TRA Suzan Mulokozi amesema kuwa, inapotokea maonyesho kama hayo wananchi wajitokeze wapate elimu kwani wataepukana na matapeli ambao hujifanya vishoka wa TRA na kuwalaghai wananchi kulipia huduma kama namba ya mlipa kodi ambayo ni bure kuipata au huwatisha kuwa hapafikiki.
Anord Deogratias mkazi wa kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba ameeleza kuwa, alikuwa haelewi kuhusu namba ya mlipa kodi lakini baada ya kupata elimu ameona ni muhimu kila mwananchi kuwa nayo hivyo ameomba namba hiyo na kupewa hapo hapo.











.jpg)
.jpg)





