Na Emmanuel Chibasa
Kwa muda mrefu wafanyabiashara
na wavuvi wa dagaa katika mwalo wa Kayenze Ndogo, wilayani Ilemela, jijini
Mwanza, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukausha na kuhifadhi dagaa kwa
ubora unaotakiwa sokoni. Utegemezi wa ukaushaji wa jadi kwa kutumia mchanga na
vichanja vya wazi umewaweka katika hatari ya kupoteza sehemu ya mazao yao, hasa
mvua zinaponyesha au hali ya hewa inapobadilika bila kutarajiwa.
Hata hivyo, teknolojia ya
kukaushia dagaa kwa kutumia nishati ya jua imeanza kubadilisha hali hiyo.
Kupitia mradi unaotekelezwa na kampuni ya Millennium Engineers, wafanyabiashara
sasa wanaweza kukausha dagaa katika mazingira yaliyodhibitiwa zaidi, kwa muda
mfupi na kwa usafi unaolenga kuboresha ubora wa bidhaa zao.
Mabadiliko haya si suala la
kutumia teknolojia mpya pekee. Pia yanaibua matumaini ya kupunguza upotevu wa
chakula, kuimarisha biashara za wavuvi na wafanyabiashara, na kuboresha
upatikanaji wa dagaa ambao ni chanzo muhimu cha protini kwa kaya nyingi nchini
Tanzania.
Hali ya hewa isiyotabirika yaongeza changamoto kwa
wafanyabiashara
Kwa wafanyabiashara wengi wa
dagaa katika mwambao wa Ziwa Victoria, ukaushaji ni hatua muhimu inayotegemea
sana hali ya hewa. Dagaa wanapokosa kukauka kwa wakati unaofaa kutokana na mvua
au unyevunyevu, wafanyabiashara wanaweza kukabiliwa na changamoto za ubora,
uhifadhi na upatikanaji wa soko.
Kabla ya kuanza kutumia
teknolojia hiyo, dagaa walikuwa wakianikwa moja kwa moja kwenye mchanga au
vichanja vya miti kando ya ziwa. Njia hizi ziliwaweka wazi kwa vumbi, uchafu,
wadudu na mabadiliko ya hali ya hewa, hali iliyoweza kuathiri usafi na ubora wa
bidhaa.
Agness Selestine, mmoja wa
wafanyabiashara wa dagaa katika mwalo huo, anasema teknolojia ya kukaushia kwa
kutumia nishati ya jua imewapunguzia changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo,
hasa wakati wa mvua.
“Dagaa sasa wanakauka haraka
na wakiwa safi zaidi, tofauti na ilivyokuwa kwa kukausha kwenye mchanga,”
anasema Agness.
Kwa upande wake, Latifa
Buchoji anasema teknolojia hiyo imeongeza matumaini ya kupata dagaa wenye ubora
unaokubalika zaidi sokoni.
Anasema ubora wa dagaa ni jambo muhimu katika biashara yao kwa sababu unaathiri namna wanavyoweza kuuza bidhaa zao na kuwafikia wanunuzi wanaohitaji viwango vya juu vya usafi.
Teknolojia ya sola inapunguza muda wa
ukaushaji
Kwa mujibu wa Mhandisi
Wistone Nnko, mtaalamu wa nishati ya jua kutoka Millennium Engineers,
changamoto za ukaushaji wa dagaa na mazingira yasiyo rafiki kwa wafanyabiashara
ndizo zilizochochea kuanzishwa kwa mradi huo.
Anaeleza kuwa awali
wafanyabiashara walitumia muda mrefu kukausha dagaa kwa njia za kawaida, huku
wakikabiliwa na changamoto za kupata mazingira safi na salama ya kufanyia kazi.
“Mradi wetu umekuja kuleta
mapinduzi katika sekta ya uvuvi Ziwa Victoria. Wavuvi na wafanyabiashara
walikuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kukausha dagaa katika
maeneo yasiyo salama na kutumia muda mrefu katika kazi hiyo.
“Tumeleta teknolojia ya
kisasa inayotumia nishati ya jua kukausha dagaa. Wanawake baada ya kununua
dagaa kutoka kwa wavuvi huwaleta hapa kiwandani, tunawapima na kuwafanyia
usafi, kisha tunawaweka kwenye kifaa maalumu cha kukaushia (solar dryer),
ambacho hutumia takribani saa tatu kukausha dagaa,” anasema Mhandisi Wistone.
Anasema teknolojia hiyo inalenga kuboresha ubora wa mazao ya dagaa na kuwasaidia wafanyabiashara kupata bidhaa zinazoweza kukidhi mahitaji ya masoko yenye viwango vya juu.
Kwa wafanyabiashara,
kupunguza muda wa ukaushaji kunaweza kuwa na umuhimu mkubwa, hasa pale hali ya
hewa inapokuwa haieleweki na muda wa kukausha unakuwa changamoto.
Hata hivyo, manufaa ya
teknolojia hiyo katika kupunguza upotevu wa dagaa na kuongeza muda wa kuhifadhi
yanahitaji kuangaliwa pia kupitia takwimu za uzalishaji, ubora na kiwango cha
bidhaa zinazoharibika kabla na baada ya matumizi ya teknolojia hiyo.
Zaidi ya ukaushaji: Taa za sola kubadilisha
shughuli za uvuvi
Mbali na teknolojia ya
kukaushia dagaa, mradi wa Millennium Engineers pia unahusisha uzalishaji na
usambazaji wa taa za sola kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
Kwa muda mrefu, baadhi ya
wavuvi wamekuwa wakitegemea taa za karabai katika shughuli zao za usiku.
Matumizi ya taa hizo yanahusisha gharama za mafuta na uzalishaji wa moshi, huku
yakileta changamoto nyingine za kimazingira.
Frank Faustine, mvuvi katika
mwalo wa Kayenze Ndogo, anasema matumizi ya taa za sola yamebadilisha namna
anavyofanya shughuli zake za uvuvi.
Anasema mwanga wa taa hizo
umemsaidia kuvutia dagaa na kuongeza mavuno yake, huku akipunguza gharama
alizokuwa akitumia kununua mafuta ya taa za karabai.
“Taa za sola zinatoa mwanga
wa kutosha unaosaidia kuvutia dagaa kwa wingi na kuokoa gharama za mafuta. Pia,
zinatusaidia kuepuka uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya taa za
karabai na betri za asidi, ambazo ni hatari kwa viumbe hai,” anasema Frank.
Hata hivyo, matumizi ya taa
hizo yanahitaji kuambatana na usimamizi endelevu wa uvuvi ili kuhakikisha
ongezeko la ufanisi wa shughuli za uvuvi haliathiri rasilimali za samaki katika
Ziwa Victoria.
Teknolojia bado haijawafikia wavuvi wote
Licha ya mabadiliko
yanayoonekana katika mwalo wa Kayenze Ndogo, teknolojia hiyo bado haijafika
katika maeneo mengine yanayozunguka Ziwa Victoria.
Katika mwalo wa Busekera,
wilayani Musoma Vijijini, na mwalo wa Makoko, Manispaa ya Musoma, baadhi ya
wafanyabiashara bado wanategemea njia za jadi za kukaushia dagaa kwa kutumia mchanga
na vichanja.
Hali hii inaonyesha tofauti
ya upatikanaji wa teknolojia kati ya maeneo mbalimbali ya uvuvi. Wakati baadhi
ya wafanyabiashara wameanza kunufaika na mifumo mipya ya ukaushaji, wengine
bado wanakabiliwa na changamoto za kutegemea hali ya hewa na mazingira ya wazi.
Kwa wafanyabiashara hao,
upatikanaji wa teknolojia rafiki kwa mazingira unaweza kuwa sehemu ya suluhisho
la kuboresha uhifadhi na ubora wa dagaa, lakini gharama za vifaa, upatikanaji
wa mitaji na miundombinu vinaweza kuwa vikwazo vya kuenea kwake.
Serikali yawekeza katika nishati safi kwa
sekta ya uvuvi
Mradi huo unatekelezwa na
Millennium Engineers kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), ambayo imechangia asilimia 30 ya gharama za utekelezaji, sawa
na shilingi milioni 560, kwa mujibu wa taarifa za mradi.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya
Nishati Jadidifu wa REA, Mhandisi Advera Mwijage, anasema mchango wa serikali
unalenga kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama katika shughuli za
kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Pia ametoa wito kwa
wawekezaji wengine kuwekeza katika teknolojia zinazotumia nishati jadidifu ili
kuwafikia wananchi katika maeneo mengine nchini.
Kwa upande wake, Mhandisi
Wistone Nnko anasema serikali inapaswa kuendelea kuweka mazingira
yatakayorahisisha upatikanaji wa vifaa vya nishati ya jua kwa gharama nafuu.
Anashauri serikali kuangalia
uwezekano wa kutoa ruzuku na kupunguza gharama za kodi kwa vifaa vinavyoagizwa
kutoka nje ya nchi ili wafanyabiashara na wavuvi wadogo waweze kumudu
teknolojia hizo.
“Naamini serikali ina malengo
mazuri katika kukuza matumizi ya teknolojia hizi. Naiomba itoe ruzuku ili vifaa
tunavyoagiza kutoka nje ya nchi vipatikane kwa gharama nafuu. Wavuvi wengi wana
nia ya kutumia teknolojia hizi lakini hawana uwezo wa kutoa fedha nyingi kwa
wakati mmoja,” anasema.
Sekta ya uvuvi ni muhimu katika usalama wa
chakula
Umuhimu wa kuboresha
teknolojia za uchakataji na uhifadhi wa dagaa unaonekana pia katika mchango wa
sekta ya uvuvi katika uchumi na lishe ya Watanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu mwaka 2023/2024, sekta ya uvuvi ni miongoni
mwa sekta muhimu zinazochangia katika Pato la Taifa, kutoa ajira na kuimarisha
usalama wa chakula.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa
sekta ya uvuvi ilikua kwa asilimia 1.9 mwaka 2022 na kuchangia asilimia 1.8
katika Pato la Taifa.
Aidha, sekta hiyo inatoa
ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni sita, ikiwemo ajira za moja kwa moja kwa
wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji 35,986.
Samaki na mazao yake pia ni
sehemu muhimu ya lishe ya wananchi, hasa kutokana na mchango wake katika
upatikanaji wa protini inayotokana na wanyama.
Kwa mantiki hiyo, kuboresha
namna dagaa wanavyokaushwa, kuchakatwa na kuhifadhiwa ni sehemu ya juhudi pana
za kuhakikisha mazao ya uvuvi yanafika kwa walaji yakiwa katika ubora unaofaa.
Je, suluhisho hili linaweza kuwafikia wavuvi
wengi zaidi?
Uzoefu wa Kayenze Ndogo
unaonyesha namna uwekezaji katika nishati jadidifu unavyoweza kusaidia kutatua
baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wavuvi.
Hata hivyo, ili teknolojia
hiyo iwe na mchango mpana katika kuimarisha usalama wa chakula na kukabiliana
na athari za mabadiliko ya tabianchi kuna haja ya kuangalia namna inavyoweza
kufikishwa katika mialo mingine, hususan maeneo ambayo wafanyabiashara bado
wanategemea ukaushaji wa wazi.
Serikali, wawekezaji na
taasisi za maendeleo wanapaswa kushirikiana kutafuta mifumo ya kifedha
itakayowawezesha wavuvi na wafanyabiashara wadogo kumudu vifaa hivyo.
Kwa wafanyabiashara wa dagaa wa Ziwa Victoria, teknolojia ya kukaushia kwa kutumia nishati ya jua inaweza kuwa zaidi ya njia mpya ya kukausha mazao. Ikiendelezwa na kupatikana kwa gharama nafuu, inaweza kuwa sehemu ya juhudi za kupunguza upotevu wa chakula, kuimarisha biashara na kujenga mifumo ya chakula inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.









