Na. Andrew Kadege, WAF - Arusha
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema huduma za tiba ya dharura zinahitaji mifumo ya afya iliyojiandaa wakati wote ili kuokoa maisha ya wagonjwa, akisisitiza kuwa katika huduma hizo hakuna nafasi ya kusubiri kwa kuwa kila dakika ni muhimu.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo Novemba 11, 2026 wakati wa kufungua rasmi Mkutano wa Nane wa Tiba ya Dharura Afrika (ACEM 2026), unaofanyika jijini Arusha, Mhe. Mchengerwa amesema tofauti na huduma nyingine za afya ambazo mgonjwa anaweza kupanga miadi ya kupata matibabu siku nyingine, huduma za dharura zinahitaji mwitikio wa haraka, akitolea mfano mama anayevuja damu baada ya kujifungua, mtoto anayepata shida ya kupumua na mwendesha pikipiki anayepata ajali usiku.
Mhe. Mchengerwa amesema mifumo ya afya inapaswa kuwa tayari kutoa huduma kabla mgonjwa hajafika hospitalini, badala ya kuanza kujiandaa baada ya dharura kutokea.
Ameeleza kuwa dhana ya huduma za tiba ya dharura ina historia ndefu, akitaja juhudi za daktari wa upasuaji wa jeshi la Ufaransa, Dominique-Jean Larrey, katika miaka ya 1790, aliyeanzisha matumizi ya magari mepesi ya kubebea majeruhi yaliyofahamika kama Flying Ambulances, ili kuwafikishia huduma za kitabibu wanajeshi waliojeruhiwa vitani bila kusubiri mapigano kumalizika.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema dhana ya Golden Hour (Saa ya Dhahabu) inayosisitiza umuhimu wa kupata matibabu ndani ya muda mfupi baada ya kupata jeraha au hali ya dharura inaendelea kuwa fundisho muhimu katika huduma za afya, kwa kuwa mara nyingi kinachosababisha vifo si jeraha au ugonjwa pekee, bali pia umbali na muda unaopita kabla mgonjwa hajafikiwa na wataalamu wenye ujuzi.
Mhe. Mchengerwa amesema thamani ya maisha ya binadamu inapimwa pia kwa namna jamii inavyojiandaa kuokoa maisha wakati wowote, ikiwemo nyakati za usiku, akisisitiza kuwa kila maisha yanapaswa kulindwa bila kujali mazingira au wakati ambao dharura imetokea.
Mhe. Mchengerwa amebainisha kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya nusu ya vifo vinavyotokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati vinatokana na hali za kiafya ambazo zinaweza kushughulikiwa kupitia huduma za tiba ya dharura.
Amesema umuhimu wa huduma hizo ulitambuliwa kimataifa mwaka 2019 kupitia Mkutano wa Baraza la Afya Duniani (World Health Assembly), uliozitambua huduma za tiba ya dharura kuwa sehemu muhimu ya huduma za afya kwa wote, na si huduma ya ziada inayopaswa kupatikana katika nchi tajiri pekee.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya huduma za tiba ya dharura ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati, hatua itakayosaidia kupunguza vifo na ulemavu unaoweza kuzuilika.
✍️wizara ya afya








