Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma
Wizara ya Afya imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Uongezaji wa Virutubishi kwenye Chakula wa mwaka 2026 pamoja na Kanuni za Uongezaji wa Virutubishi kwenye Chakula za mwaka 2024, zinazotoa msingi wa kisheria na kiutendaji kwa wasindikaji kuzingatia taratibu na viwango vinavyotakiwa.
Hayo yamesema na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakim, Agosti 13, 2026 jijini Dodoma wakati wa Hafla ya kukabidhi virutubishi vya Vitamini A na Mwongozo wa Uongezaji Virutubishi kwenye chakula wa mwaka 2026 kwa Chama cha Wasindikaji wa Maduta ya Alizeti Tanzania ( TASUPA), akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe
Amesema Wizara imekamilisha Mfumo wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Uongezaji wa Virutubishi kwenye Chakula na kununua na kusambaza mashine 12 za i-check kwa ajili ya kupima kiwango cha madini chuma kwenye unga wa ngano na mahindi katika mikoa 12 huku ikiwezesha upatikanaji wa Rapid Test Kits kwa ajili ya kupima madini joto kwenye chumvi, madini chuma kwenye unga na Vitamini A kwenye mafuta ya kula yaliyosafishwa.
Dkt. Eliud ameeleza kuwa Wizara pia imenunua lita 100 za Vitamin A Premix ambazo zinakabidhiwa kwa Chama cha Wasindikaji wa Mafuta ya Alizeti (TASUPA) kwa ajili ya kusambazwa kwa wasindikaji wadogo.
“Vilevile, Wizara imenunua na kusambaza Dosifier 160 katika mikoa 10 kwa ajili ya kusaidia wasindikaji wadogo kuongeza virutubishi kwenye unga, pamoja na mashine nne za kusafisha mafuta na kuongeza Vitamini A zinazofungwa katika vituo vya kusafishia mafuta vya Dodoma, Singida na Mbeya,” amesema Dkt. Eliud
Dkt. Eliud amesema kuwa Mwongozo huo utasaidia kuhakikisha vyakula vinavyotakiwa kuongezwa virutubishi, ikiwemo unga wa ngano, unga wa mahindi, chumvi na mafuta ya kula yaliyosafishwa, vinakuwa bora na salama kwa walaji.
Aidha, amesisitiza matumizi ya mkakati wa uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula vinavyosindikwa kama njia muhimu ya kuongeza vitamin na madini katika chakula na kukabiliana na athari za upungufu wa virutubishi hivyo mwilini.
Ameongeza kuwa mkakati huo unalenga kukabiliana na changamoto ya upungufu wa vitamini na madini ambayo imekuwa ikiathiri makundi mbalimbali katika jamii, hususan vijana wa rika balehe, wanawake walio katika umri wa uzazi na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Dkt. Eliud ameeleza kuwa upungufu wa vitamini na madini unaweza kusababisha madhara mbalimbali kiafya, ikiwemo upungufu wa damu, udumavu na ukondefu kwa watoto, pamoja na athari za kimaumbile kwa mtoto kabla ya kuzaliwa. Virutubishi hivyo pia vina mchango mkubwa katika kuimarisha afya na ustawi wa jamii.
“Tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ulaji usiozingatia mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula. Kaya nyingi hutegemea zaidi nafaka, mizizi na ndizi, huku ulaji wa vyakula vyenye vitamini na madini kwa wingi, ikiwemo matunda, mboga, nyama, samaki, maziwa na mayai, ukiwa bado mdogo,” amesema Dkt. Eliud
✍️wizara ya afya







