Na Robinson Wangaso – Musoma
Waamini wa Kanisa Katoliki kutoka Jimbo la Musoma na majimbo ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Bariadi na Bunda wameungana Agosti 13, 2026, katika Misa Takatifu ya Mazishi ya Padre Charles Mushangi Mwiguta iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Jimbo la Musoma la Bikira Maria Mama wa Mungu. Misa hiyo iliongozwa na Mhashamu Baba Askofu Flavian Kasala wa Jimbo la Geita, huku mahubiri yakitolewa na Mhashamu Baba Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo la Bunda. Mwili wa Padre Mwiguta ulizikwa katika makaburi maalumu ya Mapadre wa Jimbo la Musoma yaliyopo Seminari ya Mtakatifu Pius X Makoko.
Katika mahubiri yake, Askofu Masondole aliwahimiza waamini kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na kudumu katika imani licha ya mateso na changamoto za maisha. Alisema Padre Mwiguta alikuwa mfano wa uvumilivu na imani, hasa katika kipindi cha zaidi ya miaka minne alichokuwa akikabiliwa na changamoto za kiafya, ikiwemo kufanyiwa huduma ya kusafisha damu mara kwa mara.
Askofu Masondole alisema pamoja na maumivu aliyopitia, Padre Mwiguta hakuruhusu ugonjwa kumtenga na Mungu, bali aliendelea kushikamana na imani na kushiriki katika maisha ya Sakramenti, ikiwemo kupokea Ekaristi Takatifu. “Kila mmoja wetu aone katika kuzaliwa kwake kuwa ni zawadi ya Mwenyezi Mungu, ili kumtumikia, kuwahudumia na kushirikiana na watu mbalimbali katika ulimwengu huu,” alisema Askofu Masondole.
Askofu huyo pia alisisitiza nafasi ya familia katika malezi ya utu, imani na maadili, akisema familia ndiyo msingi wa malezi ya viongozi na watu wema katika jamii. Alisema maisha na matendo mema ya Padre Mwiguta yanapaswa kuwa urithi wa kiroho kwa Kanisa na jamii kupitia utume wake wa Upadre na huduma kwa watu wa Mungu.
Akisoma historia ya marehemu, Padre Alphonce Nyibosa alisema Padre Charles Mwiguta alizaliwa Julai 12, 1960, katika Kijiji cha Mabui Merafuru, Musoma, akiwa mtoto wa pili kati ya watoto 12 wa Faustine Magwata Mushangi na Annastazia Nyamaungo Manyama. Alibatizwa na kupokea Komunio ya Kwanza Novemba 2, 1975, katika Parokia ya Mabui na kupokea Sakramenti ya Kipaimara Oktoba 13, 1977, katika Seminari ya Mtakatifu Pius X Makoko.
Padre Mwiguta alisoma shule ya msingi Mabui Merafuru na baadaye Seminari Ndogo ya Mtakatifu Pius X Makoko. Mwaka 1982 alijiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Anthony wa Padua Ntungamo kwa masomo ya Falsafa, kabla ya kuendelea na Teolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga Segera, Dar es Salaam. Alipokea Daraja Takatifu ya Ushemasi Januari 6, 1991, na kupewa Daraja la Upadre Julai 27, 1992.
Katika utume wake, Padre Mwiguta alihudumu katika Parokia za Zanaki, Iramba, Nyegina, Kibara, Mwisenge, Mugango na Rwamlimi, pamoja na kuwa mwalimu na mlezi katika Seminari ya Mtakatifu Pius X Makoko. Pia alihudumu katika malezi ya miito na TYCS kati ya mwaka 1993 na 1997. Mwaka 2002 alitumwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania (SAUT), Mwanza, kusomea Uandishi wa Habari.
Padre Mwiguta alifariki dunia Jumapili, Agosti 9, 2026, majira ya saa moja asubuhi, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Musoma. Waamini wamemkumbuka kama Padre aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kutafakari na kufafanua Neno la Mungu kupitia mahubiri na mafundisho yake ya kina kuhusu imani na maisha ya Kikristo.
Misa ya Mazishi ilihudhuriwa na viongozi wa Kanisa, Mapadre, watawa wa kike na wa kiume, wanafamilia, ndugu, jamaa na waamini kutoka majimbo mbalimbali. Kwa niaba ya Askofu wa Jimbo la Musoma, Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila, Padre John Chacha aliwashukuru wote walioshiriki katika kumuaga Padre Mwiguta na wale waliomhudumia wakati wa ugonjwa wake.
Mazishi hayo yalihitimishwa kwa sala na ibada za Kanisa, huku waamini wakimkabidhi marehemu kwa huruma ya Mungu na kutangaza tumaini la Kikristo katika uzima wa milele. “Raha ya milele umpe Ee Bwana, na mwanga wa milele umwangazie. Padre Charles Mwiguta apumzike kwa amani. Amina.”









