Na Mwandishi Wetu, Manyara.
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara, limesema juhudi za kutokomeza mila na desturi zenye madhara kwa watoto wa kike zinapaswa kuungwa mkono na makundi yote katika jamii.
Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly, ameyasema hayo Julai 23, 2026, kwa nyakati tofauti akiwa katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari za Wilaya ya Mbulu, Mkoani Manyara. Amesisitiza kuwa, kumalizwa kwa mila hizo ni njia muhimu ya kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa na mustakabali mwema kwa siku za usoni.
Amebainisha kuwa, miongoni mwa mila zinazopaswa kukomeshwa ni ukeketaji na ndoa za utotoni. Amesema mila hizo zinaathiri vibaya maendeleo ya kitaaluma na afya kwa wasichana, na kuwanyima fursa ya kufikia ndoto zao kimaisha.
Ameongeza kuwa, suala hilo haliwezi kumalizwa na serikali pekee, bali jamii nzima inapaswa kushiriki katika mapambano hayo. Hivyo amewataka viongozi wa kidini, viongozi wa kimila, wazazi na mashirika yasiyo ya kiserikali kujitokeza kupinga vitendo hivyo na kutoa elimu kwa ufanisi inayoweka wazi madhara ya mila hizo ambazo serikali imeendelea kuzipinga kwani zinarudisha nyuma juhudi za maendeleo.
Aidha, Mkurugenzi huyo amehimiza fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wa kiume iendelee kutolewa kwa usawa katika familia, huku akiwataka wazazi na walezi kuimarisha malezi bora kwa watoto ili taifa liweze kuendelea kuwa na kizazi chenye hekima, busara na uadilifu.
Rhobi. ametoa wito kwa wadau wote wa maendeleo na wananchi kuendelea kuunga mkono kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia. Akisisitiza wanaume katika familia kuhakikisha wanashiriki vyema kukemea vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji ili kufanikisha dhamira ya serikali kuweza kuutokomeza.


