Na Angela Sebastian
Kagera: WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Rusahunga–Rusumo yenye urefu wa kilomita 92 unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili iwe kichocheo cha maendeleo ya wananchi, biashara za kikanda na ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Ulega alitoa maelekezo hayo alipokagua maendeleo ya mradi huo wa kimkakati unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 209 unaotekelezwa katika wilaya za Biharamulo na Ngara.
Alisema barabara hiyo ni sehemu ya mtandao wa barabara unaounganisha Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki, hivyo kukamilika kwake kutaimarisha usafirishaji wa watu na bidhaa ndani na nje ya nchi.
"Serikali haitaki kuona ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo inayotumia fedha nyingi za umma. Mradi huu lazima ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa," alisema Ulega.
Aidha, aliutaka mkandarasi kuhakikisha pamoja na ujenzi wa barabara, unaweka miundombinu yote muhimu ya usalama ikiwemo alama za barabarani, vivuko vya watembea kwa miguu, mifereji ya kupitisha maji na taa za barabarani ili kupunguza ajali, hasa kwa wanafunzi, wafanyabiashara, watembea kwa miguu na watu wenye mahitaji maalumu.
Pia aliwahimiza wananchi wanaoishi kandokando ya barabara hiyo kutumia fursa zitakazotokana na mradi huo kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ili kuboresha huduma za usafiri, kuchochea ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza fursa za uwekezaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ngara, Dotto Bahemu, alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutamaliza adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi kutokana na ubovu wa miundombinu.
Alieleza kuwa safari ya kilomita 60 kati ya Rusahunga na Ziroziro ilikuwa ikichukua kati ya saa nne hadi sita, hali iliyowalazimu baadhi ya wananchi kutumia njia ya kupitia Rwanda ili kufika Ngara kwa haraka zaidi.
"Barabara hii itafungua uchumi wa maeneo yetu, itarahisisha usafirishaji wa mazao, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza fursa za uwekezaji. Wananchi wa Ngara na Mkoa wa Kagera kwa ujumla wameisubiri kwa muda mrefu, hivyo tuna imani itanufaisha wananchi na kukuza shughuli za kiuchumi," alisema Bahemu.
Aliwataka pia wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali wakati wa utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhan Kido, alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha zaidi ya Sh bilioni 502 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomita 300.6 mkoani humo.
Alisema uwekezaji huo utabadilisha uchumi wa Kagera kwa kuongeza fursa za biashara, kurahisisha usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii pamoja na kuvutia wawekezaji. Aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati bila vikwazo vya kiutawala.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Hamza Faisary, alisema mradi wa Rusahunga–Rusumo ni sehemu ya Programu ya Tanzania Transport Integration Project (TanTIP), inayojumuisha miradi minne ya barabara na mitatu ya viwanja vya ndege yenye thamani ya dola za Marekani milioni 550, sawa na takribani Sh trilioni 1.5.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Festo Julius, mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa Februari 18, 2023, huku kazi zikianza Julai 5 mwaka huo. Alisema hadi sasa mradi umefikia asilimia 77 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Desemba 10 mwaka huu.
Wabunge wengine wa Mkoa wa Kagera walitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na ushirikiano ili kunufaika kikamilifu na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya maendeleo.








