Mhe. Devotha Daniel : Amani ni Msingi wa Maendeleo

0


Kagera : Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Devotha Daniel, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa utulivu wa nchi ndiyo nguzo inayowezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.

Devotha alisema maendeleo makubwa yanayoonekana nchini, hususan katika sekta ya miundombinu, yamewezekana kutokana na mazingira ya amani na utulivu ambayo yameendelea kudumishwa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali.

"Tuendelee kuitunza amani ya nchi yetu, kwani maendeleo tunayoyaona leo yanatokana na utulivu uliopo. Bila amani, miradi mikubwa ya maendeleo isingeweza kutekelezwa kwa ufanisi," alisema Devotha.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Rusahunga–Rusumo yenye urefu wa kilomita 92. Mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 209.2 na unatarajiwa kuboresha usafiri na usafirishaji, kurahisisha biashara za ndani na zile za kikanda pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kagera.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Rusahunga, Wilaya ya Biharamulo, na Benako, Wilaya ya Ngara, Devotha alisema wananchi wanapaswa kutambua na kuthamini jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo ambayo imeleta mageuzi katika sekta ya miundombinu na huduma za kijamii.

Alisema miradi hiyo imeendelea kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi, huku akisisitiza kuwa mafanikio yake yatategemea pia namna wananchi watakavyoendelea kudumisha amani, mshikamano na ushirikiano.

"Amani ndiyo msingi wa maendeleo. Miradi hii itakuwa na manufaa makubwa zaidi ikiwa wananchi wataendelea kushirikiana, kuilinda na kuitumia kwa ajili ya kuinua uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla," alisema.

Devotha pia aliwahimiza wanawake wa maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo kutumia fursa zitakazotokana na ongezeko la wasafiri na wafanyabiashara kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aliwashauri kuwekeza katika biashara za vyakula na vinywaji, kilimo cha mbogamboga, pamoja na kuuza bidhaa za asili zinazozalishwa katika Mkoa wa Kagera, akieleza kuwa wasafiri wanaotumia barabara hiyo kuelekea nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki watakuwa soko muhimu la bidhaa hizo.

"Barabara hii siyo tu njia ya usafiri, bali ni kichocheo cha ajira, biashara na ongezeko la kipato kwa wananchi. Ni muhimu kutumia fursa hizi kujikwamua kiuchumi na kuboresha ustawi wa familia,"Devotha 

Aidha, Devotha alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa miundombinu ya barabara mkoani Kagera, akieleza kuwa uwekezaji huo unaendelea kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na maendeleo ya kijamii kwa wananchi wa mkoa huo.






Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top