Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imehitimisha operesheni maalumu dhidi ya kilimo cha bangi katika Wilaya za Tarime na Rorya, mkoani Mara, ambapo mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 291.2 yameteketezwa.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema leo Julai 24, 2026 kuwa katika operesheni hizo, Mamlaka pia imekamata magunia 15 ya bangi kavu pamoja na pikipiki nne zilizokuwa zikitumika katika shughuli hizo haramu. Watu wawili wamekamatwa, huku uchunguzi ukiendelea kuwabaini na kuwakamata washirika wengine waliohusika katika mtandao huo.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema operesheni endelevu zinazotekelezwa na Serikali zimechangia kupungua kwa kilimo cha bangi katika Mkoa wa Mara kwa takribani asilimia 80. Mwaka 2024, zaidi ya ekari 3,500 za mashamba ya bangi ziliteketezwa mkoani humo, hatua iliyosaidia kudhoofisha uzalishaji wa bangi katika maeneo yaliyokuwa yameathirika zaidi.
Amesema matokeo ya operesheni hizo yanaonesha kuwa juhudi za Serikali zinaendelea kuzaa matunda, huku wananchi wengi wakianza kuachana na kilimo cha bangi na kuelekeza nguvu zao katika shughuli halali za uzalishaji zinazowanufaisha wao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Chanzo : DCEA








