Na Robinson Wangaso – Mara
Kanisa la Anglican Tanzania, Dayosisi ya Rorya, limewataka waamini wake kuwa mfano wa kuigwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na utunzaji wa mazingira ili kulinda uoto wa asili na kuhifadhi uumbaji wa Mwenyezi Mungu.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Anglican Tanzania, Dayosisi ya Rorya, Askofu Moses Yamo, wakati wa maadhimisho ya miaka 16 tangu kuanzishwa kwa Dayosisi hiyo yaliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro Kowak Saye, mkoani Mara.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa kipindi cha wiki moja kuanzia Julai 23 hadi 26, 2026, yakihusisha waamini kutoka Dayosisi mbalimbali nchini Tanzania na kutoka nje ya nchi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Askofu Yamo alisema Kanisa lina wajibu wa kuhubiri Injili sambamba na kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia miradi ya uzalishaji mali na uhifadhi wa mazingira.
Alisema miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Dayosisi hiyo ni mashamba ya kilimo, upandaji miti, ufugaji wa kuku pamoja na miradi ya elimu inayolenga kuinua ustawi wa jamii.
"Shamba letu la kilimo lililopo Kijiji cha Ryagoro limekuwa chachu ya mabadiliko ya maisha kwa waamini na wananchi wanaoishi katika eneo hilo. Vilevile, mradi wa upandaji miti wa Ryagoro umechangia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara huku ukihifadhi mazingira na kuendeleza uumbaji wa Mwenyezi Mungu," alisema Askofu Moses Yamo.
Aliongeza kuwa Dayosisi hiyo inaendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ikiwemo ufugaji wa kuku, shule za awali na shule ya msingi kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto wa Wilaya ya Rorya na maeneo mengine.
Kwa mujibu wa Askofu Yamo, mafanikio ya Kanisa yanategemea zaidi mshikamano na uwezo wa waamini kujitegemea badala ya kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili wa nje.
"Tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha miaka 16 ya Dayosisi yetu. Nawataka wachungaji wote wawe nguzo imara katika parokia zao kwa kuanzisha miradi ya maendeleo na kujitegemea. Ni wakati wa kuacha kutegemea wafadhili wa nje, kwani hali imebadilika na misaada si ya uhakika kama ilivyokuwa zamani," alisema.
Aidha, aliwataka waamini kuendelea kuchangia kwa hiari ujenzi wa shule mpya unaoendelea chini ya Dayosisi hiyo ili kutoa fursa zaidi za elimu kwa watoto.
"Tumeanza ujenzi wa shule yetu na tunategemea zaidi michango ya Wakristo wetu. Tukishikamana na kushirikiana, tutatimiza ndoto hii ambayo itanufaisha watoto wetu na jamii kwa ujumla. Viongozi wa Kanisa na waamini wote tushikamane ili kuendelea kulijenga Kanisa letu na kuliletea maendeleo endelevu," alisisitiza.
Kwa upande wao, baadhi ya waamini wa Dayosisi ya Rorya walisema miradi ya kilimo na upandaji miti imeleta manufaa makubwa kwa jamii kwa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Hawa Gunda na Jacton Ochieng, ambao ni waamini wa Dayosisi hiyo, walisema miradi hiyo imewanufaisha si waamini wa Kanisa la Anglican pekee bali wananchi wote wanaoizunguka Dayosisi.
"Miradi hii imetuletea manufaa makubwa. Tumepata mbegu bora za mazao, tumeongeza uzalishaji mashambani na wananchi wengi wamejifunza umuhimu wa kuhifadhi mazingira kupitia upandaji miti. Haya ni maendeleo yanayogusa jamii nzima," walisema.
Maadhimisho ya miaka 16 ya Dayosisi ya Rorya yalitumika pia kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake na kuweka mikakati ya kuimarisha huduma za kiroho, elimu, kilimo, utunzaji wa mazingira na maendeleo ya kijamii kwa manufaa ya waamini na wananchi kwa ujumla.









