Na Happyness Hans, WAF – Morogoro
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeanza kuhuisha Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Wagonjwa wa Magonjwa ya Virusi Vinavyosababisha Kutokwa na Damu (Viral Hemorrhagic Fevers), hatua inayolenga kuweka utayari wa Tanzania ili kuzuia na kudhibiti milipuko ya magonjwa hatari ikiwemo Ebola na Marburg.
Akizungumza Julai 27, 2026 mkoani Morogoro, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dkt. Michael Kiremeji, amesema mwongozo uliopo uliandaliwa mwaka 2019 ukiwa umejikita zaidi kwa ugonjwa wa Ebola, hivyo umeonekana kuwa na umuhimu wa kuboreshwa ili kuendana na ushahidi wa kisayansi na mapendekezo mapya ya WHO.
Dkt. Kiremeji amesema maboresho hayo yataleta mwongozo mmoja wa kitaifa utakaowawezesha wataalamu wa afya kuboresha utambuzi, matibabu na usimamizi wa wagonjwa wa magonjwa yote ya virusi vinavyosababisha kutokwa na damu, ikiwemo Ebola na Marburg.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Serikali ya kuimarisha ulinzi wa afya ya umma kwa kuhakikisha watumishi wa afya wanakuwa na ujuzi, vifaa na miongozo sahihi ya kukabiliana na milipuko kabla haijatokea.
Kwa upande wake, mwakilishi wa (WHO) amesema maboresho ya mwongozo huo yataongeza uwezo wa Tanzania wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko kwa kuzingatia viwango na mapendekezo ya kisasa ya shirika hilo.
Kikao hicho kimewakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili, KCMC, Hospitali za Rufaa za Kanda za Bugando na Mbeya, UDOM, JKCI, UDSM Kampasi ya Mbeya, Kibong'oto, Muhas pamoja na wadau kutoka WHO, CDC na AMREF.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali za kuimarisha mfumo wa afya nchini na kuongeza uwezo wa taifa wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na kulinda afya ya wananchi.
✍️wizara ya afya


