Serikali Yaombwa Kuongeza Wigo wa Elimu Kuhusu Malaria kwa Watu Wenye Ulemavu

0


Na Atley Kuni, WAF – Morogoro

Watu wenye ulemavu wameiomba Serikali, kupitia Wizara ya Afya, kuongeza wigo wa utoaji wa elimu, huduma na ushirikishwaji katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ili kuhakikisha kila mtu anapata fursa ya kuchangia maendeleo ya taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rai hiyo imetolewa  Julai 29, 2026, mkoani Morogoro wakati wa kikao cha kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa watu wenye ulemavu. Kikao hicho kilihusisha kikosi kazi kutoka Wizara ya Afya na wadau mbalimbali, kilichofika kuzungumza na kundi hilo kwa lengo la kupata maoni kuhusu namna bora ya kuboresha jumbe za elimu ya malaria ili ziwe jumuishi na ziwafikie wananchi wote.

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoa wa Morogoro, Salum Ramadhani Ally amesema ni muhimu Wizara ya Afya kushirikiana kwa karibu na chama hicho ili kuhakikisha taarifa sahihi kuhusu malaria zinawafikia watu wenye ulemavu wa kusikia kwa wakati.

"Tunaiomba Wizara ya Afya ishirikiane na Chama cha Viziwi Tanzania ili taarifa sahihi zitufikie kwa wakati. Tuna mtandao mkubwa unaotuwezesha kuwasiliana kwa haraka nchini kote," alisema Ally.

Kwa upande wake, Blesing Thobias Kadaya amesema watu wenye ulemavu wa kusikia hukumbana na changamoto wanapofika katika vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama. Amesema hali hiyo husababisha baadhi ya watoa huduma kushindwa kuelewa mahitaji yao, jambo linalochelewesha au kuathiri upatikanaji wa huduma stahiki.

Ameiomba Serikali kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa na wakalimani wa lugha ya alama ili kurahisisha mawasiliano kati ya wagonjwa wenye ulemavu wa kusikia na watoa huduma.

Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, Mkuu wa Dawati la Habari katika Programu ya Taifa ya Kudhibiti Malaria, (NMCP) Wizara ya Afya, Bi. Leah Ndekule, amesema lengo la kukutana na watu wenye ulemavu ni kusikiliza changamoto wanazokutana nazo na kupata maoni yatakayosaidia kuboresha jumbe za elimu kuhusu malaria.

Hapo awali tuliandaa jumbe za elimu kuhusu malaria, lakini tulibaini kuwa hazikuwafikia ipasavyo baadhi ya makundi, hususan watu wenye ulemavu. Ndiyo maana tunafanya zoezi hili ili kuhakikisha tunakuwa na mawasiliano jumuishi yanayomfikia kila mwananchi bila kuacha kundi lolote nyuma," amesema Ndekule.

Aliongeza kuwa kikosi kazi kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu– TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), pamoja na wadau mbalimbali, kipo mkoani Morogoro kwa siku tano kikikusanya maoni na kuandaa vifaa vya mawasiliano vinavyozingatia makundi yote ya jamii.

Vifaa hivyo ni pamoja na video za elimu, vipeperushi na jumbe mbalimbali za uelimishaji kuhusu malaria zitakazowezesha wananchi wote, wakiwemo watu wenye ulemavu, kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

✍️wizara ya afya










Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top