Na OR-MV, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana imeendelea na mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu maboresho ya Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa, ambapo Juni 24, 2026 imekutana na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaowawakilisha vijana katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Msekwa C, Bungeni jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ha Rais-Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na kisera yaliyotokea tangu kutungwa kwa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa mwaka 2015, Serikali imeona umuhimu wa kuwa na sheria itakayozingatia mazingira ya sasa na kukidhi mahitaji ya vijana.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, Bi. Tunu Emily Temu, amesema kuwa mchakato huo umelenga kupata maoni yatakayosaidia kujenga Baraza la Vijana lenye nguvu na uwezo wa kukidhi matarajio ya vijana na wadau wa maendeleo ya vijana nchini, huku akibainisha kuwa baadhi ya vipengele vya sheria iliyopo ya Baraza la Vijana la Taifa, Sura ya 441 havijaendana na muundo wa sasa wa Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaowawakilisha vijana, Mhe. Zainab Athuman Katimba, amempongeza Waziri Mhe. Joel Arthur Nanauka, kwa kuendeleza maboresho hayo ambayo yatakuwa sehemu muhimu ya kuandaa sheria itakayowezesha kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa lenye ufanisi zaidi.
✍️wizara ya maendeleo ya vijana


_1782323266.jpeg)
_1782323220.jpeg)

