Na Robinson Wangaso, Musoma
Wananchi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara wameahidiwa kurejeshewa huduma ya maji safi katika hali yake ya kawaida baada ya kukumbwa na mgao wa maji kwa zaidi ya wiki tatu kutokana na hitilafu za kiufundi katika mfumo wa uzalishaji na usambazaji wa maji.
Ahadi hiyo imetolewa na Afisa Uhusiano na Habari wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Chausiku Marwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya semina iliyoandaliwa na EWURA.
Chiku alisema changamoto hizo zilisababishwa na hitilafu ya umeme katika mitambo ya uzalishaji maji ya Bukanga pamoja na kupasuka kwa bomba kubwa la kusambaza maji.
Alieleza kuwa tatizo la umeme tayari limetatuliwa kwa kushirikiana na TANESCO, huku mafundi wa MUWASA wakiendelea na matengenezo ili huduma irejee kwa wananchi wote.
Awali, baadhi ya wananchi walilalamikia upungufu wa maji uliodumu kwa muda mrefu, hali iliyowalazimu kutafuta huduma hiyo katika maeneo mengine huku wakihoji kuendelea kulipia ankara za maji licha ya huduma kutokuwa ya uhakika.
Chiku aliwataka wananchi kuwa na subira akieleza kuwa mfumo wa usambazaji unahitaji muda kujaza mtandao mzima wa mabomba kabla huduma haijarejea kikamilifu.
Akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Nyirabu Musira, aliwataka wananchi kutumia mifumo rasmi ya kuwasilisha malalamiko kuhusu huduma za maji na nishati, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi, watoa huduma na EWURA katika kuboresha utoaji wa huduma nchini.



