Wizara ya Kilimo imetoa elimu ya mwongozo wa matumizi ya ghala za umma katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya tarehe 11 hadi 24 Mei 2026 kwa lengo la kuwajengea wakulima na wadau wa sekta ya kilimo uelewa kuhusu matumizi sahihi ya ghala za umma ili kuhakikisha mazao yanahifadhiwa kwa usalama na ubora unaotakiwa.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Usindikaji na Uongezaji Thamani, Mhandisi Godwin Makori amesema kuwa mwongozo unalenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kulinda ubora wa mazao, kuongeza thamani yake sokoni na kuhakikisha wakulima wanapata manufaa zaidi kutokana na uzalishaji wa na kusaidia kuimarisha matumizi ya maghala ya umma na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
“Elimu ya mwongozo wa matumizi ya ghala za umma ni muhimu kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kwani ushiriki wa kila mdau katika kuzingatia mwongozo huu utasaidia kujenga mfumo imara wa uhifadhi na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini,” amefafanua zaidi Mhandisi Makori.
Wakulima waliopatiwa mafunzo wameahidi kutumia elimu waliyoipata kwa vitendo kwa kufuata mwongozo uliotolewa, hatua ambayo itasaidia kupunguza upotevu wa mazao, kuongeza ubora wa mazao na kuboresha kipato chao pamoja na maendeleo ya sekta ya kilimo kwa ujumla.
✍️wizara ya kilimo


