Kikwete Ashiriki Mkutano Mkuu wa TAPSEA- Arusha

0


 Na Ghati Msamba

WAZIRI  wa Ofisi ya Rais,Utumishi wa Umma na utawala Bora,Ridhiwani Kikwete ameshiriki ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Ngurdoto, mkoani Arusha.  

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emanuel Nchimbi, na umehudhuriwa na wanachama zaidi ya 5,050 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma pamoja na taasisi binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Makamu wa Rais Nchimbi amewataka wajumbe wa TAPSEA kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na mshikamano wakati wa uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho. 

Amesisitiza kuwa umoja na uadilifu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taasisi yoyote na kwamba viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kuwa mfano bora wa uwajibikaji na uzalendo katika kulitumikia taifa.

Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa taaluma ya uandishi na uendeshaji wa ofisi katika kuimarisha utendaji kazi serikalini na katika taasisi mbalimbali nchini.

 Amesema waandishi waendesha ofisi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha mawasiliano, utunzaji wa kumbukumbu na ufanisi wa shughuli za kila siku za ofisi vinafanyika kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

 Waziri Ridhiwani ,Kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, alipata fursa ya kuzungumza na wajumbe wa mkutano huo ambapo aliwakumbusha kuhusu juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini.

Alieleza kuwa Serikali imeendelea kupandisha madaraja ya watumishi, kuboresha miundo ya utumishi na vyeo mbalimbali, pamoja na kulipa madeni ya mishahara na stahiki nyingine zilizokuwa zikidaiwa kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi wake ili kuongeza morali na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kwamba  katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha maslahi ya watumishi na kwamba jitihada hizo zitaendelea kadri uwezo wa kiuchumi na mapato ya Serikali yatakavyoruhusu.

Mkutano huo wa TAPSEA unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya chama, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha taaluma ya waandishi waendesha ofisi nchini.

 Pia mkutano huo utahitimishwa kwa uchaguzi wa viongozi wapya watakaoongoza chama hicho kwa kipindi kijacho.






Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top