Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amesema Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano na Canada katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija kwa manufaa ya pande zote mbili.
Akizungumza Aprili 15, 2026 jijini Dodoma wakati wa mazungumzo na ujumbe wa Chama cha Wabunge Wastaafu wa Canada (CAFP) ulioongozwa na Mhe. Yasmin Ratansi, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuinua mchango wa kilimo katika uchumi wa taifa.
Ameeleza kuwa maeneo ya ushirikiano yanajumuisha tafiti za kilimo, ubadilishanaji wa wataalamu, maendeleo ya umwagiliaji, matumizi ya mitambo ya kisasa, pamoja na uwekezaji katika mazao ya kimkakati na uzalishaji wa mbolea. Hatua hizo zinatarajiwa kuongeza ubora wa mazao na ushindani katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mhe. Ratansi amesema Canada iko tayari kushirikiana na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kutumia Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo (IDRC) kuimarisha tafiti na ubunifu katika kilimo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa takwimu sahihi za wakulima ili kuwezesha upangaji bora wa miradi, huku akihimiza ushiriki wa moja kwa moja wa wakulima, kuimarishwa kwa vyama vya ushirika, na matumizi ya fursa za biashara ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima.
✍️wizara ya mambo ya nje








