NEMC kwa kushirikiana na Kampuni ya SWECO AB ya Sweden, wamesaini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa mradi wa kubadili taka kuwa nishati tarehe 16 Aprili 2026 katika ofisi za NEMC, jijini Dar es Salaam.
Upembuzi huo yakinifu utatekelezwa katika Mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza na unafadhiliwa na Shirika la maendeleo la Swedfund AB kutoka Sweden.
Lengo la mradi huu ni kuchochea ukuaji wa uchumi rejelezi na kufanya taka kuwa fursa, hususan taka ozo, kwa kuzigeuza kuwa rasilimali yenye kuweza kutumika kwa ajili ya kuzalisha umeme au kuzalisha mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo magari katika maeneo ya mijini.
Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza katika kukabiliana na changamoto ya ongezeko la taka zinazozalishwa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Kupitia mradi huu, NEMC inaendelea kusisitiza usimamizi endelevu wa taka, utenganishi wa taka katika vyanzo na matumizi bora ya rasilimali kwa ajili ya kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kijani.
✍️Nemc






