Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetangaza kuzindua rasmi Mfuko wenye jumla ya Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuwawezesha vijana wanaojihusisha na sekta ya ubunifu nchini.
Akizungumza jijini Arusha Machi 11, 2026, Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Paul Makonda amesema mfuko huo unatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ukiwa na lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sekta hizo.
Amewataja wanufaika wa mfuko huo kuwa ni pamoja n watengeneza maudhui mtandaoni (content creators), wasanii, wanamuziki, waigizaji, waandishi wa habari, influencers pamoja na wabunifu wa kazi mbalimbali za sanaa.
Waziri Makonda amesema awali Wizara ilikuwa imepangiwa Shilingi Bilioni 20, lakini baada ya mazungumzo na Benki ya CRDB, kiwango hicho kimeongezwa na kufikia jumla ya Bilioni 50 ili kupanua wigo wa vijana watakaonufaika na mfuko huo.
Ameeleza kuwa, kwa sasa kinachosubiriwa ni tarehe rasmi ya uzinduzi wa mfuko huo, ambapo baada ya uzinduzi fedha hizo zitaanza kutolewa kwa vijana waliopo katika sekta ya habari, sanaa na ubunifu ili kuwawezesha kukuza kazi zao na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi na kutumia vipaji vyao kama chachu ya maendeleo ya Tanzania.
✍️wizara ya habari, utamaduni, Sanaa na michezo










