#UleviSioDili : Mirungi ni moja ya dawa za kulevya zinazochochea ubongo kufanya kazi kwa kiwango kisicho cha kawaida na mara nyingi huonekana na wengi kama nyongeza ya nguvu au burudani ya muda mfupi, Lakini nyuma ya msisimko huu kuna hatari zinazoshika moyo unaopiga haraka, usingizi unaopotea, migongano na migogoro na hata madhara makubwa kwa afya ya uzazi .
Wataalam wa maswala ya afya wanaeleza kuwa watu wanaotumia mirungi mara kwa mara, hupoteza kidogo kidogo uwezo wa mwili na akili kuendeleza maisha ya kawaida. Vile vile, jamii inayokumbwa na tatizo hili hususani vijana ina hatari ya kupoteza nguvu kazi, amani na ustawi wa kila siku. Kutambua madhara yake ni hatua ya kwanza ya kulinda afya, familia na mustakabali wako.
Kwa mujibu wa shirika la ICCAO Tanzania, Mirungi ni aina ya dawa za kulevya inayochochea mfumo wa fahamu kufanya kazi kuliko kawaida na usababisha mapigo ya moyo na upumuaji kuongezeka. Kemikali zinazoathiri ubongo ni cathinone na cathine na mirungi kwa watumiaji au vijana wengi ufahamika kama gomba, miti, gati, mronge, veve, miraa au mbaga.
Kama ulikua unatumia au kama ulikua unapanga kutumia na ulikua ufahamu madhara ya mirungi, basi fahamu ya kwamba matumizi ya mirungi yana madhara kwa watumiaji ikiwa ni pamoja na;
1. Huongeza shinikizo la damu na kusababisha kiharusi
2. Huathiri mfumo wa uzazi kwa kupunguza nguvu za kiume, ugumba pamoja na utasa
3. Ajali za barabarani kwa wanaotumia vyombo vya moto kutokana na kukosa usingizi
4. Magonjwa ya afya ya akili yanayojitokeza kwa vipindi vya mwezi mchanga
5. Husababisha vidonda kwenye mfumo wa chakula na saratani
6. Kuozesha na kubadilisha rangi ya meno, maumivu ya fizi na harufu mbaya mdomoni
7. Husababisha magonjwa ya ini
8. Hupunguza hamu ya kula
9. Husababisha kukosa choo na kusababisha bawasiri
10. Husababisha uchovu mkali na sonona
11. Husababisha ukatili, fujo, ugonvi na migogoro
12. Husababisha kushuka kwa uzalishaji na kipato.
Elimu hii ya madhara ya madhara ya Mirungi kwa binadamu na jamii inaletwa kwenu na shirika la ICCAO Tanzania kupitia mradi wa Ulevi Sio Dili kwa kushirikiana na Musoma News Hub
✍️Imeandikwa na Emmanuel Chibasa
Chanzo: ICCAO Tanzania
#UleviSioDili
#UleviSioDiliVijanaTuamke
#EpukaUleviLindaAfyaYako
#ICCAOTanzania
#MusomaNewsHub

.png)
