Katika kuendelea na kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetoa semina ya uwekezaji mkoani Rukwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wananchi na wafanyabiashara kuhusu fursa na vivutio vya uwekezaji vinavyopatikana nchini.
Semina hiyo ilifunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, ambaye aliwataka wananchi wa Rukwa kuipokea na kuitumia ipasavyo elimu ya uwekezaji inayotolewa na TISEZA kwa maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Mhe. Makongoro Nyerere alisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa ndani akisema:
“Mtanzania akifanya uwekezaji, anabaki Tanzania kwa manufaa ya Tanzania. Tofauti na uwekezaji unapofanywa na mgeni na kurudisha faida nchini kwake kwa faida ya nchi yake.”
Kwa upande wa TISEZA, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji, Bw. Daudi Riganda, aliwasilisha mada iliyofafanua kwa kina kuhusu historia na majukumu ya TISEZA, sababu za kuhamasisha uwekezaji, pamoja na faida za kuwekeza nchini.
Wasilisho hilo pia lilielezea miundombinu wezeshi ya uwekezaji, vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi, makundi ya wawekezaji, sekta za vipaumbele, fursa zilizopo, vigezo vya kujisajili na kupata cheti cha vivutio na leseni, pamoja na taratibu na maboresho mbalimbali yaliyofanyika kwa mujibu wa sheria.
Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalijibiwa kwa ufafanuzi wa kina na wataalamu wa TISEZA.
Aidha, katika jitihada za kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusogeza huduma karibu na wananchi, TISEZA ilizindua rasmi Dawati la Uwekezaji mkoani Rukwa. Afisa dawati alikabidhiwa vitendea kazi rasmi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.





