Na Hassan Kimweri, WAF - Morogoro
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeziagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa, Taifa, Wilaya na Vituo vya Afya kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ametoa maagizo hayo leo Februari 25, 2026 mkoani Morogoro wakati akizungumza na Waganga Wakuu Wafawidhi na watendaji wa vituo vya kutoa huduma vinavyofanya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa (Sentinel Surveillance Centers).
"Tunaendelea kuviwezesha vituo vingi zaidi katika ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa hasa ukusanyaji wa sampuli mapema na kuziwasilisha mapema maabara ya Taifa, kazi hii ni ulinzi wa nchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hakuna mbadala”, amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe ameiasa jamii kuacha matumizi holela ya dawa za “Antibiotiks” ili kudhibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa, jambo linalopelekea wengi kushindwa kupona baada ya kutumia baadhi ya “antibiotiks”
"Mtu akijisikia mafua, kikohozi vimeambatana na homa, mwili kuchoka, kuumwa kichwa nk anakimbilia duka la dawa kununua antibiotiki, hiyo sio sawa, ukihisi unaumwa nenda kwenye kituo cha tiba wakwambie unaumwa nini baada ya kupimwa badala ya kunywa dawa kiholela” amesema Dkt. Magembe.
Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesema licha ya ugonjwa wa Kipindupindu kuisha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na magonjwa hayo ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, matumizi sahihi ya vyoo na kutumia maji safi na salama.
Pia, Dkt. Magembe ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na Shirika la Kimataifa la PATH.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko kutoka Wizara Dkt. Vida Mmbaga amesema, Tanzania imejenga uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
✍️wizara ya afya








