Na Emmanuel Chibasa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Inatarajia kuanza majaribio ya matumizi ya teknolojia mpya ya utangazaji wa redio kidijitali nchini unaofahamaika pia kama Digital Sound Broadcasting(DSB)
Dkt. Bakari Jabir ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Akizungumza katika Mkutano wa mwaka wa Watoa huduma za Utangazaji(ABC 2026) jijini Dodoma, amesema hatua hiyo imefikiwa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kuimarisha utangazaji hususani katika maeneo ya vijijini.
Amesema kwa Sasa wamekamilisha maandalizi yote ya udhibiti na watoa huduma tayari wamepatikana kwa ajili ya kuanza hatua za majaribio katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Dodoma, Mbeya na Dar es Salaam.
Awali akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwijuma amesema katika kuhakisha watoa Fursa wezeshi kwa watengeneza maudhui mtandaoni, Serikali imeshusha malipo ya ada ya leseni kutoka shilingi 500,000 hadi shilingi 50,000 huku malipo ya ada ya maombi yakishuka Hadi shilingi 10,000 pekee
Amesema mabadiliko hayo pia yanahusisha kundi la wakusanyaji wa maudhui mtandaoni (online Content Aggregators), ambao maombi ya ada ya leseni imeshushwa kutoka shilingi 1,000,000 hadi shilingi 100,000.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, hadi kufikia Decemba 2025 wamefanikiwa kutoa jumla ya leseni za Utangazaji 707 huku leseni za Maudhui Mtandaoni zikiwa ni 318.
Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma za Utangazaji (ABC 2026) Unafanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa New Generation Hall kwa muda wa siku mbili kuanzia Februari 12 na 13 , huku kauli mbiu ikiwa ni "Matumizi ya Teknolojia katika Kupanua na Kuboresha Huduma za Utangazaji Vijijini".

















