Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Februari 12, 2026 limevifungia viwanda vya Juye Concrete Company Limited na YK Tosh Company Limited vilivyopo Mikocheni jijini Dar es Saalam vinavyojihusisha na uzalishaji wa zege, kufuatia ukiukwaji wa masharti ya kisheria ya mazingira.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya timu ya wataalamu wa mazingira kutoka NEMC kufanya ukaguzi katika viwanda hivyo na kubaini mapungufu mbalimbali ya kimazingira.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC), Bw. Hamadi Taimuru, amesema kuwa changamoto zilizobainika ni pamoja na kuanzisha shughuli za uzalishaji bila kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM), kukosekana kwa miundombinu ya kudhibiti vumbi, pamoja na ukosefu wa mfumo wa kutibu maji taka yanayozalishwa kiwandani, hali iliyosababisha maji hayo kutiririka katika maeneo ya makazi ya wananchi bila kutibiwa.
Bw. Taimuru alieleza kuwa NEMC ilishawahi kufanya ukaguzi katika viwanda hivyo zaidi ya mara nne na kutoa maelekezo ya maandishi na mdomo ili kufanya marekebisho ya miundombinu hiyo. Hata hivyo, maelekezo hayo hayakutekelezwa jambo linalosababisha malalamiko kutoka kwa majirani kuendelea na hivyo kusababisha Baraza kuchukua hatua ya kuvifungia viwanda hivyo ili vipate muda wa kuweza kutekeleza kikamilifu masharti yote yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria.
Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC), Bi. Glory Kombe, amewataka wawekezaji wote kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kabla ya kuanza kwa miradi yao ili kupata ushauri wa kitaalamu mapema, kuzingatia sheria na kuepusha madhara kwa mazingira na afya ya jamii.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Juye Concrete Company Limited, Bw. Cao Zhojun, ameihakikishia NEMC kuwa kampuni yake itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinaendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na viwango vya kimazingira.
NEMC itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kwa lengo la kulinda mazingira na afya ya wananchi, huku ikihakikisha kuwa shughuli za maendeleo na uwekezaji zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya uendelevu na uwajibikaji wa kimazingira.
chanzo : nemc







