Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 12 Februari, 2026 amewapokea Wataalamu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) waliyokuja kumtambulisha Mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 78 kwa gharama ya shilingi bilioni 38, 228,813,559.32.
Akizungumza katika hafla fupi ya kumtambulisha mkandarasi, Mhe. Mtambi amesema kwa sasa vijiji vyote 458 vya Mkoa wa Mara vimepata umeme na mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na utapeleka huduma za umeme katika vitongoji 78 vilivyoko katika Wilaya zote sita za Mkoa wa Mara.
“Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 nchi nzima inakuwa na umeme hadi katika ngazi ya vitongoji” amesema Mhe. Mtambi na kuongeza kuwa hiyo ni ishara ya mwanga, matumaini na maendeleo katika sekta zote.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa uchaguzi kwa Watanzania ambazo Mhe. Mtambi amesema zinaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa.
Kanali Mtambi amesema Mkoa wa Mara ni miungoni mwa mikoa inayoendelea kunufaika na miradi ya maendeleo inayowawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kupata huduma za msingi na kuelezea furaha yake katika mradi huo ambao amesema anategemea utakuwa chachu ya maendeleo katika vitongoji hivyo.
Mhe. Mtambi ameipongeza REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha maeneo yote ya Tanzania yanapata umeme mapema iwezekanavyo na kumtaka mkandarasi wa mradi huo kutekeleza mradi huo kwa muda uliopangwa ili wananchi waweze kupata huduma za umeme kwa haraka.
Kwa upande wake Meneja wa Miradi REA Kanda ya Ziwa Mhandisi Ernest Mkale amesema REA imejipanga kimkakati kuhakikisha matarajio ya Mhe. Rais yanafikiwa na imejipanga kusimamia mradi huo ili utekelezwe kwa ubora na muda uliopangwa.
Aidha, Mhandisi Mkale amesema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa miaka mitatu na kwa wakati wote wataalamu wa REA watamsimamia mkandarasi kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaenda kama ulivyopangwa.
“Serikali italipia gharama kubwa katika utekelezaji wa mradi huo na utakapokamilika wananchi watachangia shilingi 27,000 kama gharama ya kawaida ya kuunganisha umeme katika maeneo ya vijijini” amesema Mhe. Mkale.
Mhandisi Mkale pia amemtambulisha Mkandarasi wa mradi huo Shahidu Rutakolezibwa kutoka katika Kampuni ya Namis Cooperative Limited ambaye atatekeleza mradi huo na kukabidhi orodha ya vitongoji 78 kutoka katika Wilaya za Musoma, Bunda, Butiama, Tarime, Serengeti na Rorya vitakavyofikiwa na mradi huo katika vitongoji vya Mkoa wa Mara
Hafla ya kumtambulisha mkandarasi imefanyika katika ukumbi wa uwekezaji, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na imehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, viongozi wa dini, Maafisa wa REA, TANESCO.
chanzo: ofisi ya mkuu wa mkoa Mara


