Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amekutana na Waziri wa Katiba na Sheria, Haki za Binadamu na Masuala ya Jinsia wa nchini Burundi, Mhe. Alfred Ahingejeje katika ofisi za Wizara - Mtumba, jijini Dodoma tarehe 18 Februari 2026 ambapo ujumbe huo ulitaka kupata uzoefu wa hatua mbalimbali zilizopigwa katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini Tanzania.
Waziri Ahingejeje amemabatana na ujumbe wa wataalamu mbalimbali kutoka Serikali ya Burundi, wakiwemo wataalamu kutoka Shirika la CARE International Burundi; pamoja na wawakilishi wa CARE International Tanzania.
Ujumbe huo ulipata wasaa wa kutembelea Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa Njia ya Mawasiliano cha Wizara ya Kilimo kilichopo katika Viwanja vya John Malecela- Nanenane, jijini Dodoma ambapo Katibu Mkuu Mweli alieleza matumizi ya teknolojia katika Sekta ya Kilimo kutoka kilimo cha mazoea na kuwa nchi inayojikita kwenye kilimo biashara huku ikitekeleza mbinu zote zinazotakiwa katika kuinua kilimo na mkulima.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinaenda kisasa zaidi ambapo mbali na kuwa na maafisa ugani wanaowafikia wakulima moja kwa moja lakini kuna njia za kidigitali za kuwafikia wakulima kama vile kuwahudumia kwa njia ya simu ambapo wakulima na wadau wengine wa kilimo wanapiga simu na kutatuliwa changamoto zao. Lakini pia kila afisa ugani amepewa kifaa cha kupimia afya ya udongo (soil scanner) inayomwezesha kupima afya ya udongo kwa mkulima; huku pia kuna njia ya kidigitali inayoiwezesha Wizara kufuatilia pikipiki zilizotolewa kwa wakulima kote nchini ili kufanya kazi iliyopangwa,” amesema Bw. Mweli.
Pia Bw. Mweli ameeleza zaidi kwa Waziri Ahingejeje kuwa Serikali ya Tanzania inazidi kuboresha utolewaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima wote wake kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa mazao hatua ambayo imeleta tija kubwa kwenye kilimo. Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha Sekta ya Kilimo kwa kuongeza bajeti maradufu kwenye utafiti, uzalishaji wa mbegu, umwagiliaji huku ikiimarisha masoko ya ndani na nje ya nchi kwa wakulima.
Naye Waziri Ahingejeje mbali na kushukuru mapokezi na elimu ya kilimo kutoka kwa Katibu Mkuu Mweli, ameielezea Tanzania kama sehemu muhimu kwa Burundi katika kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya kilimo huku akisisitizia kuwa Burundi itaendelea kujifunza kutoka Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina ardhi kubwa ya kulimo na imeboresha kilimo chake.
✍️wizara ya kilimo


