Chama cha Wakala wa Pembejeo Tanzania Chatakiwa Kuimarisha Upatikanaji wa Pembejeo Bora

0


Chama cha Wakala wa Pembejeo Tanzania (TANADA) kimepewa wito kuimarisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe, wakati akifungua kikao cha kufufua chama hicho tarehe 18 Februari 2026, katika Hoteli ya Royal Village, jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa TANADA, iliyoanzishwa mwaka 2009 na kusajiliwa rasmi 2010, ilidhoofika kutokana na changamoto za rasilimali na uendeshaji, jambo lililoonesha haja ya chama hicho kuwa na misingi imara ya uongozi, usimamizi na vyanzo vya mapato vinavyojitegemea.

Pia Prof. Msoffe amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa Sekta ya Kilimo kipaumbele kama mhimili wa uchumi wa Taifa, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya kilimo chenye tija yanategemea uwepo wa mawakala wa pembejeo wenye weledi na uwajibikaji.

Naye Mratibu wa Programu ya Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi yaani Agricultural and Fisheries Development Programme (AFDP), Bw. Clemence Shio, amesema kuwa  Serikali kupitia Mradi wa AFDP imeanza mchakato wa kufufua TANADA kwa kuandaa katiba yake mpya, kupanua uwakilishi kuanzia Wilaya hadi Taifa, na kuweka utaratibu wa kupata viongozi wa mpito watakaoongoza mchakato wa uhuishaji.

Ameongeza kuwa kupitia Programu ya AFDP, mawakala wa pembejeo watapatiwa mafunzo na kujengewa uwezo ili waweze kutoa huduma bora, salama na zenye kuaminika kwa wakulima, hatua itakayoongeza ufanisi katika mnyororo wa thamani wa kilimo na kuchochea uzalishaji wenye tija.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mpito wa TANADA, Bw. Gerold  Mlenge, ameishukuru Serikali kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kufufua chama hicho na kuahidi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha TANADA inakuwa taasisi imara, inayojitegemea na yenye kuleta manufaa kwa wanachama wake pamoja na wakulima kwa ujumla.

✍️wizara ya kilimo

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top