Waziri wa Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekemea tabia ya watendaji wa Serikali kupokea matatizo ya wananchi kama salamu badala ya kuyatatua kwa kufanyia kazi ipasavyo.
Amesema hayo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa majimbo ya Bumbuli, Mlalo na Lushoto, waliojitokeza wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku tano katika Mkoa Tanga tarehe 17 Februari 2026.
Kuhusu hoja za upatikanaji wa skimu za umwagiliaji, Waziri Mkuu Nchemba amewaondoa shaka wananchi hao na kueleza kuwa skimu nne za umwagiliaji katika jimbo la Mlalo tayari zimeshafanyiwa usanifu na hatua za ujenzi zitafuata.
Aidha, katika kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo na mbegu za kilimo, naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amewaeleza wananchi hao kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) itapeleka tani 500 za mbegu bora za ngano ili kusaidia wakulima wa Lushoto kama walivyoomba.
Naibu Waziri Silinde ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu bora za mahindi kwa wakulima msimu wa kilimo wa 2025/2026.


