- Awaonya viongozi wa vijiji na Serikali kwa ujumla
- Ataja maslahi binafsi ndiyo tatizo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka viongozi ngazi mbalimbali nchini kuheshimu mipaka asili kwenye maeneo ya ardhi husika sambamba na kuwataka wananchi kuepuka kutumia madalali wakati wa mchakato mzima wa kupata hatimiliki za ardhi.
"Viongozi wa vijiji, viongozi ngazi mbalimbali wanaopotosha mipaka huku wakijua mipaka yetu ya asili ni hapa, waache tabia hiyo kwa sababu huko nikumgombanisha Mheshimiwa Rais na wapiga kura wake", amesema Kaspar Mmuya Naibu Waziri.
Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo tarehe 16 Februari 2026 wakati wa hafla ya ugawaji wa Hakimiliki za Kimila (CCROs) zaidi ya 1,300 iliyofanyika katika Kijji cha Namagondo, wilayani Ukerewe zilizoandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa wakazi wa vijiji vya Namagondo na Busiri vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza.
Amesema, baadhi ya viongozi wanapogundua fursa zilizopo karibu na maeneo ya ardhi husika hususan kwenye mipaka kama ya minada na madini mara moja huanza kusogeza mipaka yao na baadaye kusababisha mgogoro.
Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza kuanzia tarehe 13 hadi 18 Machi 2026 kwa ajili ya zoezi la Kiliniki ya Ardhi jijini Mwanza, kukabidii hakimiliki za kimila Wilaya ya Ukerewe pamoja na halmashauri ya Buchosa katika Kijiji cha Kasisa.


