Tarehe 25 Februari 2026, Mkurugenzi wa Ujengaji uwezo na Haki za Binadamu LHRC, Deogratius Bwire, ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Asasi ya Haki za Binadamu katika Chuo cha Ustawi wa Jamii – Bamaga, Dar es Salaam.
Akiwa mmoja wa wazungumzaji katika hafla hiyo, Wakili Bwire amewahimiza wanachama wa asasi hiyo mpya kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea haki za binadamu, si tu kwa manufaa yao binafsi bali kwa jamii nzima. Ameeleza kuwa jamii yenye haki na usawa inajengwa na vijana wenye ujasiri wa kusimama dhidi ya ukiukwaji wa haki bila kupepesa macho.
Katika hotuba yake, ameeleza nafasi ya LHRC katika kuwawezesha vijana kuwa watetezi wa haki za binadamu kupitia elimu ya kisheria na mafunzo ya ujasiri wa kiraia. Amebainisha kuwa LHRC, kama mwanzilishi na mlezi wa Vilabu vya Haki za Binadamu nchini Tanzania, imefanikiwa kuanzisha zaidi ya vilabu 300 kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, ambapo vijana waliopitia vilabu hivyo wamekuwa chachu ya kusimamia sauti za wanyonge katika jamii.
Aidha, Wakili Bwire ameikaribisha asasi hiyo mpya kushirikiana kwa karibu na LHRC, kwa kupata elimu ya msaada wa kisheria pamoja na mafunzo ya haki za binadamu, akisisitiza kuwa milango ya LHRC iko wazi wakati wote kwa vijana.
Kwa upande wao, wanafunzi wanachama wa asasi hiyo wameipongeza LHRC kwa mchango wake mkubwa katika kulinda na kutetea haki za binadamu nchini, huku wakitaja mifano ya kesi mbalimbali ambazo LHRC imefanikiwa kusaidia wananchi kupata haki zao.
chanxo: LHRC








