Na Said Said WMJJWM, Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua Mkakati wa Jubilei wa World Vision Tanzania wa miaka mitano (2026–2030) unaolenga kuboresha ustawi na maendeleo endelevu ya watoto, familia na jamii nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 25 Februari 2026, Waziri Gwajima amesema mkakati huo ni nyenzo muhimu kwani unatarajia kuwafikia watoto milioni 3.4 walio katika mazingira magumu zaidi nchini, huku ukiimarisha mifumo ya kitaifa inayohudumia zaidi ya Watanzania milioni 22.
Waziri Dkt. Gwajima amepongeza Shirika la World Vision Tanzania kwa mchango wake katika sekta mbalimbali ikiwemo ulinzi wa watoto na wanawake, afya na lishe, elimu, kilimo, uchumi wa kaya, maji na usafi wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ameeleza kuwa miradi ya Shirika limetumia zaidi ya shilingi bilioni 3.5 katika wilaya za Korogwe na Pangani mkoani Tanga pekee, na kuwafikia walengwa zaidi ya 15,000.
Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Gwajima amezindua Mfuko wa Mtoto Kwanza (Mtoto Kwanza Fund) wenye lengo la kubadilisha maisha ya watoto kwa kukusanya rasilimali zitakazosaidia moja kwa moja watoto na familia zilizo katika mazingira magumu. Aidha, alizindua pia mpango wa maji safi ujulikanao kama Mapping the Blue Thread, unaolenga kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama katika jamii mbalimbali nchini.
Vilevile, Waziri Gwajima ametoa maelekezo na kuahidi kuwa Wizara itaendelea kuimarisha uratibu, ushirikiano na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), ili kuimarisha uwajibikaji, kuonesha matokeo chanya ya utekelezaji wa miradi hiyo
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vision Tanzania, James Anditi, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa kwa Shirika hilo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini huku akisema kupitia mkakati uliozinduliwa, Shirika hilo linaamini litafikia watoto na familia wengi zaidi walio katika mazingira magumu
✍️maendeleo ya jamii











