Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kutoa ufadhili wa kusoma Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Takwimu , Akili Unde na Sayansi Shirikishi kupitia mpango wa _Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+)_ ambapo tayari wanafunzi kumi wamepata ufadhili huo na watasoma katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha.
Kupitia ufadhili huo pia wanafunzi wengine kumi wanatarajia kusoma kozi hizo ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Taasisi ya Indian Institute of Technology IIT Madras kampasi ya Zanzibar.
Akizungumza na Waadishi wa Habari Leo Februari 25,2026 jijini Dodoma Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema uamuzi wa kusomesha wanafunzi hao ngazi ya Uzamili ni kutokana na mahitaji ya nchi na kwamba Serikali imetenga Sh. bilioni 5 kuwezesha utekelezaji wake.
Waziri Mkenda ametumia fursa hiyo kuwaalika wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia ufadhili wa masomo kupitia Samia Scholarship.
Aidha wanafunzi waliopata ufadhili kupitia Samia Scholarship ngazi ya shahada ya kwanza wanaalikwa kuangalia majina yao kupitia Tovuti ya Wizara www.moe.go.tz, Tume ya sayansi na Teknolojia Tanzania http://www.costech.or.tz/ na Taasisi ya Afrika Ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela https://www.nm-aist.ac.tz
✍️wizara ya elimu, Sayansi na teknolojia








