Na Happynes Hans WAF - ARUSHA
Wizara
ya Afya kupitia Idara ya Kinga na Mpango wa Taifa wa Chanjo, kwa kushirikiana
na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na wadau wa sekta ya afya, inaendelea
kutekeleza afua za utoaji na uhamasishaji wa huduma za chanjo nchini ikiwa ni
mpango wa kuzidisha msukumo kwa maslahi ya jamii
Hayo yamesemwa na Afisa
Programu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bi. Lotalis Gadau, leo Februari 20,
2026, jijini Arusha, wakati wa kikao kazi cha kukamilisha rasimu ya Mkakati wa
Mawasiliano na Elimu kwa Umma kuhusu Huduma za Chanjo.
Bi. Gadau amesema
Mkakati wa Mawasiliano wa Chanjo una mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa
wananchi, kuondoa hofu na mashaka, na kuhamasisha matumizi ya huduma za
chanjo.
Amesema mkakati huo
husaidia kujenga imani kwa mfumo wa afya, kuchochea mabadiliko chanya ya tabia,
na kufikia makundi magumu ndani ya jamii kupitia vyombo vya habari kama redio,
mikutano ya kijamii na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs).
“Mkakati wa mawasiliano
wa chanjo utawawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu aina na umuhimu wa
chanjo, na kupunguza upotoshaji, hofu na mashaka yanayotokana na uvumi au imani
potofu,” amesema Bi. Gadau.
Ameeleza kuwa Wizara ya
Afya ina jukumu la kitaifa la kuboresha huduma za chanjo kwa kutunga sera,
miongozo na mikakati; kuratibu Mpango wa Taifa wa Chanjo; kufuatilia usalama wa
chanjo (AEFI) pamoja na kujenga uwezo wa watoa huduma za afya katika
mawasiliano rafiki kwa jamii.
Naye Msimamizi wa Chanjo
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bi. Rosalia Arope, amesema TAMISEMI ni
kiungo muhimu kati ya sera za kitaifa na utekelezaji wake ngazi ya jamii.
"TAMISEM inasimamia
utekelezaji wa huduma za chanjo katika mikoa na halmashauri, kuratibu huduma
ngazi ya mkoa na wilaya, kuhamasisha viongozi wa mitaa, pamoja na kuwezesha
mikutano ya kijamii na kampeni za uhamasishaji, hivyo, TAMISEMI huhakikisha
mkakati wa mawasiliano unawafikia wananchi moja kwa moja" amesema Bi.
Arope
Kwa upande wake Mratibu
wa Mabadiliko ya Tabia za Kijamii kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumba, amesema
UNICEF ina mchango katika sekta ya afya kwa kutoa msaada wa kifedha na
kitaalamu kwa programu ya chanjo, kuendeleza mikakati ya mawasiliano inayolenga
jamii (SBCC na RCCE), kufanya tafiti za kubaini sababu za baadhi ya wananchi
kusita au kukataa huduma za chanjo.
✍️Wizara ya afya


