Na Angela Sebastian
Bukoba : Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Devotha Daniel, ametoa msaada wa shilingi milioni moja kwa mtoto Grecseous Raphael mwenye umri wa miezi minne mkazi wa Kata ya Kihanga, Wilaya ya Karagwe, anayesumbuliwa na uvimbe kichwani, ili kumwezesha kufikishwa Hospitali ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya upasuaji.
Mbali na msaada huo wa fedha, Devotha pia ameahidi kugharamia bima ya afya kwa familia nzima ya mtoto huyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na ulinzi wa matibabu.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Devotha katika kuwatumikia wananchi kwa vitendo, kuwagusa wenye mahitaji maalum, na kuendelea kuleta matumaini mapya kwa jamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Devotha amesema Kuwa alipata taarifa za mtoto huyo kupitia matangazo ya kituo cha redio ya jamii cha Fadeco Radio, ambapo mama wa mtoto alikuwa akiomba msaada kwa wasamaria wema. amesema baada ya kusikia taarifa hizo, aliguswa na kuamua kufika moja kwa moja kwa familia hiyo ili kujionea hali halisi na kutoa mchango wake.
Mbali na msaada wa fedha taslimu, Devotha pia ameahidi kugharamia bima ya afya Kwa wote Katika familia nzima ili kuwawezesha kupata huduma za matibabu kwa urahisi pindi wanapohitaji.
Kwa upande wake, mama wa mtoto Swaumati Sijaji amemshukuru Mbunge huyo kwa kufika nyumbani kwao na kuwafariji pamoja na kutoa msaada huo ambao utasaidia kumpeleka mtoto wao katika Hospitali ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe huo.
Familia ya mtoto huyo kwa ujumla ilieleza kuguswa na kitendo hicho, ikisema msaada huo umewapa matumaini mapya ya kuona mtoto wao anapatiwa matibabu stahiki na kurejea katika hali ya kawaida. Walisema hawakutarajia kupata msaada kwa haraka kiasi hicho, na wakaahidi kuendelea kumuombea Mbunge huyo ili aendelee kuwahudumia wananchi kwa moyo wa huruma.
Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Karagwe Georgiana Mkapapa amesema Kuwa kitendo hicho kinaonesha namna Mbunge huyo alivyo karibu na wananchi wake, na kuwataka wanawake na wananchi kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono na kumuamini katika jitihada zake za kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.





