Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe amefanya ziara ya kutembelea shamba la vijana wanaonufaika na Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) tarehe 21 Februari 2026, Chinangali, jijini Dodoma, kwa lengo la kujionea utekelezaji wa programu hiyo na kuzungumza na vijana kuhusu mafanikio na changamoto wanazokutana nazo.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa AMCOS ya Chinangali, Bw. Peter Madukwa amesema kuwa programu hiyo imewajengea vijana uwezo wa utaalamu katika shughuli za kilimo ili kupata kupato na ajira.
Aidha, Bi. Julieth Jonas, mnufaika wa Programu ya BBT, ameishukuru Serikali kwa kumpa fursa ya kushiriki katika programu hiyo, akieleza kuwa ana matarajio makubwa ya kupata mafanikio yenye tija kupitia kilimo. Ameshauri wakulima kuzingatia kilimo cha Alizeti kwa kuwa kina manufaa makubwa kiuchumi.
Mnufaika mwingine Bw. Mtengwa Wema Mtengwa amesema kuwa Serikali imewafanyia mambo makubwa ikiwemo kuwapeleka katika Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI) kwa miezi mitano kupata mafunzo ya mbinu bora za kilimo, pamoja na mafunzo ya miezi miwili katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Ameongeza kuwa alipata pia fursa ya kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kuongeza ujuzi katika uzalishaji na masoko ya nje ya nchi, hatua iliyomjengea uwezo wa kuendesha kilimo kwa mtazamo wa kibiashara zaidi.
Baada ya kuwasikiliza vijana wa BBT, Prof. Msoffe amewaeleza kuwa Serikali ilianzisha Programu ya BBT kwa dhamira ya dhati ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya sekta ya kilimo. Ameeleza kuwa programu hiyo imejengwa katika mfumo wa mafunzo ya kisasa kupitia moduli za kisayansi na kilimo-biashara, hatua inayolenga kuongeza tija, ajira na mchango wa vijana katika uchumi wa taifa.
Ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Programu ya BBT katika maeneo yote nchini hasa katika Halmashauri, kwa lengo la kuwainua vijana kiuchumi na kuifanya sekta ya kilimo kuwa mhimili imara wa maendeleo ya Taifa.
✍️wizara ya kilimo


