Na WMJJWM-Dodoma
Serikali yaendelea na juhudi za kuchochea Maendeleo katika jamii kupitia afua mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu juu masuala ya mila na desturi zinazozofaa na zile zisizofaa kupitia mikakati mbalimbali hususani kupitia kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Jamii Neema Ndoboka alipokua akifungua kikao cha wadau wanaotekeleza eneo la mila na desturi katika Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili zidi ya wanawake na watoto(MTAKKUWA) Septemba 17,2025 Mkoani Dodoma.
Neema amewaasa wadau wa Maendeleo wanaotekeleza eneo hilo kuongeza juhudi zaidi na kutokukata tamaa kwani suala la jamii kukubali kuachana mila walizorithishwa vizazi baada ya vizazi si jambo jepesi.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango wenu katika kuleta mabadiliko katika jamii lakini suala mila na desturi linachukua muda hivyo mnapaswa kutokukata tamaa na inabidi muendelee kupambana zaidi kutoa elimu kwa wanajamii na madaliko yatakuja tu” amesema Ndoboka.
Vilevile Ndoboka ametoa wito kwa jamii kukumbatia mila na desturi zinazofaa kwani baadhi ya mila ndiyo asili ya mwafrika na zina umuhimu wake katika kulinda maadili na mienendo ya Jamii.
“Tunachokipinga ni mila zinazokandamiza na kuumiza baadhi ya makundi katika jamii kwani tunaelewa kwamba kuna mila na desturi ambazo zinazofaa na zinajenga misingi ya jamii husika na maadili ya kitanzania”amesema Ndoboka.
Kwa upande Wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Carlos Gwamagobe amewaahidi wadau hao wa maendeleo kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufikia malengo yao ya kuhakikisha mabadiliko chanya yanapatikana katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Chanzo: maendeleo ya jamii