Jaji Mkuu Ahimiza Ushirikiano kwa Wadau wa Mahakama Kuwezesha Utoaji Haki Mapema Ipasavyo

0


📌 Ni katika Mkutano wa Wadau kuhusu ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani

📌 Asisitiza pia uwajibikaji wa wadau wa mnyonyoro wa haki

📌Ashauri mikutano hiyo kufanyika angalau mara nne kwa mwaka 


Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewahimiza Wadau wa Mahakama nchini juu ya umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na mahusiano ili kutekeleza jukumu la utoaji haki mapema ipasavyo na kwa ustawi wa wananchi.

Akizungumza  tarehe 24 Septemba, 2025 wakati akifungua Mkutano wenye ajenda kuu ya Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju amesema ushirikiano na mshikamano ni wa lazima na ni takwa la kikatiba, kisheria na hata Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

“Nawashukuru Viongozi kwa kutenga muda wenu kuja kushiriki katika mkutano huu muhimu, niseme tu kwamba ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu yetu mahakamani umejengwa kwenye Katiba na kwenye sheria mbalimbali zinazoanzisha Taasisi zetu hizi, kwa hiyo ni ushirikiano wa kulazimika na wala sio wa hiari, na wote sisi nia yetu ni ustawi wa wananchi” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, kila mdau wa mnyonyoro wa haki ni muhimu, kunapokuwa na ushirikiano na uhusiano wa namna hiyo kwa wadau, kuna umuhimu mkubwa ambao ni pamoja na kuyaimarisha, kutambua mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zinazokabili ushirikiano na mahusiano hayo na kuziwekea mikakati ya kuzitatua.

“Niseme tu kwamba wajibu wetu wa kuwajibika kutekeleza yale ambayo kila mmoja wamejiwekea au yale ambayo tumewekewa kwa mujibu wa sheria ni wajibu wa kikatiba, nitarejea Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoanzisha uwajibikaji kwa kila mwananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sisi pia tuliopo Serikalini,” amesema Jaji Mkuu.

“Kwahiyo mambo haya yanatuhusu sisi wote, sisi wote tumewekwa na wananchi kwa ajili ya kuwatumikia ili kufikia ustawi wao, tumepewa majukumu ya uwajibikaji, tunapotekeleza majukumu yetu na sisi sasa tunazungumza kwenye huu mnyonyoro wa haki ambao unaishia mahakamani, Ibara ya 25 ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema wajibu wa kushiriki kazini,” ‘Kazi pekee ndio huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu na kila mtu anao wajibu (a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali na (b) kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja na yanayotakiwa na yaliyowekwa na sheria,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju ameeleza kwamba, Taasisi zote ikiwemo Mahakama zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu kuimarisha ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu mahakamani.

Aidha, Jaji Mkuu ameongeza kwa kushauri kuwa, vikao hivyo viwe endelevu na vifanyike angalau mara nne kwa mwaka (kila robo mwaka) ili kupata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama na wadau wake na hatimaye kupata suluhisho ya changamoto mbalimbali kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuzitatua ili kusonga mbele.

Kadhalika, Mhe. Masaju amesema kwamba mkutano huo umekuja wakati muafaka, ambapo kuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambapo msingi mkuu wa Dira hiyo ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu na moja ya kipaumbele cha kwanza ni Utawala Bora na Haki, kipaumbele cha pili ni Serikali za Mitaa Imara na zenye ufanisi na cha tatu ni Utumishi wa Umma unaowajibika na kipaumbele cha nne ni Amani, Usalama na Utulivu. Amesema wadau wote ni wahusika katika kusimamia na kutekeleza masuala hayo.

Aidha, Jaji Mkuu amesisitiza juu ya utumishi wa umma unaowajibika kwa kutoa rai kwa wadau hao kuwa, kila mmoja anawajibika kutekeleza malengo ya kudumisha utawala bora kwenye utekelezaji wa upatikanaji wa haki mahakamani na amani, usalama na utulivu.

Aidha Mhe. Masaju amerejea ukurasa wa 63 wa Dira hiyo ambao unahimiza ushirikiano katika sekta mbalimbali, inasema ‘ili kuhakikisha Dira 2050 inatekelezwa kwa ufanisi, Serikali imeweka mfumo imara wa usimamizi unaozingatia malengo yake mahsusi, mfumo huu umekusudia kuhimiza uwajibikaji, ukihitaji uongozi mahiri na ulio makini katika ufuatiliaji, aidha mfumo unahimiza matumizi ya mbinu zinazotoa matokeo yanayopimika.’

‘msingi wa mkakati huu ni mabadiliko makubwa ya kifikra yakilenga vitendo badala ya maneno na matokeo badala ya ahadi, uongozi, taasisi pamoja na watendaji na wadau wote wanapaswa kuwajibika ili kutimiza malengo ya Dira kwa ufanisi, Taasisi imara na mifumo Madhubuti inayolenga kuondoa uzembe, inayohimiza uwajibikaji na kuchochea ufanisi itakuwa nguzo kuu ya utekelezaji wa Dira 2050...Dira imeweka mfumo madhubuti wa utawala unaohakikisha utekelezaji unafanyika kwa nidhamu, sera zinasomana, taasisi zinakuwa imara, taasisi na wadau wote wanashirikiana.’

Amesema kwamba, mkutano huo utakuwa pia kichocheo kwa taasisi nyingine kuandaa mikutano kama huo na kuwashirikisha wadau muhimu katika sekta ya sheria inayohusu utoaji haki. Kwa kuwa ushirikiano ni muhimu katika kufikia maendeleo endelevu na matokeo yenye manufaa.

Aidha, Jaji Mkuu amesisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano ili mashauri yaweze kukamilika mapema ipasavyo huku akigusia mashauri ya jinai, mashauri ya kodi, mashauri ya biashara, mashauri ya migogoro ya kibenki na mengine.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewaomba Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kufuatilia na kuandaa taarifa kuhusu utekelezaji wa Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, ili kujua kama kweli mashauri hayo yanamalizika ndani ya miezi sita.

“Tunatengeneza pia Kanuni ambazo zitawezesha mashauri yanayosikilizwa na Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya wao nao Mahakama na washtakiwa wawe nao wanapata ushahidi wa upande wa kesi za mashtaka ili iwasaidie na wao kujitetea kwa ufanisi ipasavyo, haitoshi tu kwamba kumpa haki ya kusikilizwa lakini akiwa hana taarifa za tuhuma na ushahidi uliopo dhidi yake hapo hakutakuwa na haki ya kusikilizwa aliyopewa itakuwa imenyofolewa kwa kiasi fulani na itakuwa inakiuka Ibara ya 13 ya Katiba inayotaka usawa mbele ya sheria,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Ameeleza kuwa, kupatikana kwa kanuni hizo kutawezesha kuimarisha umakini katika upelelezi, kupunguza ubambikizaji wa mashauri, italeta umakini katika utoaji haki, itadhibiti vitendo vya rushwa, itaendana na na Katiba ambayo inataka usawa mbele ya sheria na itasaidia kupunguza mahabusu na wafungwa magerezani.

Mhe. Masaju amewaomba ushirikiano wadau hao, kuwa huru kutoa maoni yao katika mkutano huo nak weka mikakati thabiti itakayoboresha utendaji kazi ya utoaji haki na hatimaye Mahakama ya Tanzania iwe moja kati ya mihimili yenye hadi duniani.

Naye Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba amesema kufanyika kwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Nguzo namba tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2020/2021-2024/2025 ya Kuimarisha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.

“Kupitia nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama, tumesisitizwa juu ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya haki kama mhimili muhimu unaoimarisha misingi ya utawala bora. Katika utekelezaji wa nguzo hii, hivi karibuni tumeshuhudia juhudi zako za dhati Mheshimiwa Jaji Mkuu juu ya kuimarisha dhana nzima ya ushirikishwaji wa wadau. Ushiriki wako katika matukio mbalimbali, ikiwemo ziara uliyofanya Gereza Kuu Isanga tarehe 10 Julai, 2025, ufunguzi wa mjadala wa kitaifa juu ya maboresho ya sheria na sera tarehe 19 Agosti, 2025, ufunguzi wa kikao kazi baina ya ofisi ya DPP, DCI, PCCB na DCEA tarehe 20 Agosti, 2025, ufunguzi wa mkutano wa tisa wa kamati ya utatu tarehe 25/08/2025, na mengineyo mengi, unathibitisha juhudi hizo,” amesema Mhe. Kagomba.

Kaimu Jaji Kiongozi huyo amesema, kupitia ushirikiano wa dhati baina ya Mahakama na wadau, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na wadau wote waliokusanyika katika mkutano huo, utajenga taswira moja ya utumishi wa haki na kuongeza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa utoaji wa haki.

Mkutano huo wenye ajenda kuu ya Ushirikiano na mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani umehudhuriwa na wadau mbalimbali ambao ni Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi Wa Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Inspekta Generali wa Polisi, Ofisi ya Kamishna wa Magereza, Ofisi ya Kamishna wa Uhamiaji, Ofisi ya Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi Ya Kamishna wa Mamlaka Kudhibiti na Kupambana na Dawa Za Kulevya, Ofisi ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali na Ofisi ya Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Chanzo: mahakama ya Tanzania









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top