Ghati Msamba,Musoma.
MKUU wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amezindua rasmi mpango wa kilimo kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) katika shamba la Bugwema, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, huku vijana na wanawake 289 wakigawiwa maeneo ya ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa zao la mpunga ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Uzinduzi huo uliofanyika Novemba 5, 2026, ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo cha kisasa na biashara ya kilimo, kuongeza uzalishaji wa chakula pamoja na kutengeneza fursa za ajira na kipato.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Chikoka amesema kuanza kwa shughuli za kilimo katika eneo hilo ni hatua muhimu katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa wananchi wa halmashauri hiyo, hususan vijana wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji.
Amesema kupitia mpango huo, vijana watanufaika kwa kuongeza maarifa, ujuzi na matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kuongeza tija na kupata mavuno mengi.
Aidha, amewataka vijana waliopewa maeneo hayo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha mashamba hayo yanakuwa mfano wa kuigwa kwa wakulima wengine.
"Serikali imewekeza kwenu na inatarajia kuona matokeo chanya. Mashamba haya yanapaswa kuwa mfano wa darasa ili wengine waweze kujifunza na kuiga kutoka kwenu," amesema Chikoka.
Katika hatua nyingine, amewataka wanufaika hao kuwa walinzi wa miundombinu iliyowekwa katika mashamba hayo ili kuhakikisha inatunzwa na kuendelea kutumika kwa muda mrefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Pia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuhakikisha mabonde yote yanayofaa kwa kilimo yanatumika kuzalisha zao la mpunga ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa wananchi.
Amesisitiza kuwa kila kaya inapaswa kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali, huku akihimiza upandaji wa miti mitano kwa kila kaya kama sehemu ya juhudi za kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Kelvin Ruge, amesema lengo la mpango huo ni kuwafikia vijana na kuwawezesha kujihusisha na kilimo biashara ili kuongeza ajira, kipato na kujenga uchumi imara kupitia sekta ya kilimo.
Amesema kupitia programu ya BBT, Serikali inalenga kukuza kilimo cha kisasa na kuongeza fursa za ajira, ambapo ifikapo mwaka 2030 inatarajiwa kutengeneza ajira milioni 1.6 na kunufaisha watu milioni 10 katika vijiji 12,000 vya Tanzania Bara.
Aidha, amesema programu hiyo inalenga kutambua na kuendeleza biashara 200,000 za kilimo zinazomilikiwa na vijana.
Akifafanua hatua zilizofikiwa, Ruge amesema hadi sasa programu hiyo imefika katika halmashauri 162 na vijiji 6,094, huku watu 909,709 wakifikishiwa huduma kupitia mpango huo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kuchimba visima 395 vitakavyokuwa na uwezo wa kumwagilia ekari 16,662.
Amesema pia ekari 500 zimeidhinishwa katika halmashauri hiyo, kati ya ekari 100,036 zilizoidhinishwa katika halmashauri 27 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.
Naye Kaimu Mratibu wa Mpango wa BBT, Kassim Kusaya, amesema programu hiyo imeanzishwa kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana katika sekta ya kilimo, ikiwemo ukosefu wa ardhi na mitaji ya kuanzisha shughuli za uzalishaji.
Amesema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yalionesha umuhimu wa kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya wananchi, hivyo Serikali ikaona kuna haja ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.
"Katika uzalishaji, vijana wanakosa rasilimali nyingi kwa kuwa hawana ardhi. Wanapoenda benki kuomba mikopo, wanashindwa kupata kwa sababu hawana dhamana," amesema Kusaya.
Amefafanua kuwa mpango huo umekuja kuwawezesha vijana kupata ardhi na fursa za kufanya kilimo chenye tija, ambapo hadi sasa halmashauri 27 zimeidhinisha maeneo ya mashamba na kuandikisha vijana ambao wanakabidhiwa ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa mazao mbalimbali, ikiwemo mpunga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Masinono, Dismas Oongo, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo katika eneo lao, akisema utakuwa chachu ya maendeleo na utasaidia vijana kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo.
Amesema wananchi wameupokea mradi huo kwa mikono miwili kwa kuwa unaenda kutatua changamoto ya ukosefu wa ardhi na kuongeza fursa za ajira na kipato kwa vijana na wanawake.
Ameeleza kuwa uwepo wa mradi huo pia utachochea maendeleo ya kijiji kupitia shughuli za uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika sekta ya kilimo.










