RUJAT kurejesha hadhi ya Uandishi wa Habari za Vijijini

0


 Na Angela Sebastian, Dodoma   

👉Yataka wanahabari kuacha kutegemea taarifa kwa vyombo vya habari, wajikite kuibua changamoto na kuleta suluhisho 


CHAMA cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) kimeweka mikakati ya kuwajengea uwezo wanachama wake ili waweze kuandika habari zenye ubora, zinazogusa maisha ya wananchi, kuibua changamoto zinazowakabili na kupendekeza suluhisho kwa ajili ya kuleta maendeleo katika jamii.

Katibu Mkuu wa RUJAT, Prosper Kwigize, alieleza hayo wakati akitoa taarifa ya maendeleo na mikakati ya chama hicho katika mkutano mkuu uliofanyika jijini Dodoma, ambapo pia wanachama walichagua viongozi wapya watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne.

Kwigize alisema kuwa mpango huo ni miongoni mwa mikakati muhimu ya chama katika kukuza weledi, uelewa na uwezo wa wanahabari kuandika habari za uchunguzi na maendeleo zinazobainisha changamoto za wananchi na kuibua majibu yake.

Alisema RUJAT inalenga kuwa na waandishi wa habari za vijijini wanaojiamini, wenye heshima na wanaoweza kuandika habari zenye ubora na mvuto, badala ya kutegemea taarifa kwa vyombo vya habari (press release) kama chanzo pekee cha habari.

"Tunakwenda kujenga RUJAT ya waandishi wa habari za vijijini wanaojiamini, watakaojijengea heshima kwa kuandika habari zinazowauza. Hatupaswi kusubiri press release ili tuandike habari leo tumekuwa waandishi wanaotegemea taarifa hizo badala ya kujituma kutafuta habari," alisema Kwigize.

Alisisitiza kuwa taarifa kwa vyombo vya habari zinapaswa kuwa kichocheo cha kupata mawazo mapya ya habari, kufanya utafiti na kuibua habari zilizochambuliwa kwa kina, zenye tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Alitoa mfano wa barabara zinazojengwa katika maeneo ya vijijini ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha shughuli za wananchi, ikiwemo kupunguza muda wa kufuata huduma mbalimbali.

Alisema pamoja na manufaa hayo, mafanikio kama hayo mara nyingi hayapewi nafasi inayostahili katika vyombo vya habari, huku baadhi ya waandishi wakijikita zaidi katika kuandika taarifa wanazopatiwa badala ya kwenda uwanjani kutafuta habari zinazogusa maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachama wa RUJAT, Devotha Martine, Mutayoba Arbogast na Suzy Butondo, waliunga mkono mkakati huo, wakisema utasaidia kurejesha ari, ubunifu na kujituma.

Walisema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya waandishi kutokuwa wabunifu na kutofanya utafiti wa kutosha kabla ya kuandika habari, hali inayosababisha kupungua kwa habari zinazogusa maisha ya wananchi.

Akizungumzia suala hilo, Martine alisema miongoni mwa sababu zinazochangia kudorora kwa ubora wa habari ni uzembe wa baadhi ya waandishi na kukosekana kwa juhudi za kutosha katika kutafuta habari zinazojitegemea.

"Ukiangalia miaka ya nyuma, waandishi walikuwa wanajituma na kuandika habari zilizolenga kusaidia jamii na kuleta maendeleo. Lakini sasa wengi tumejikita mijini na kusubiri RPC atuite ndipo tupate habari tunapaswa kubadilika," alisema.

Aliongeza kuwa mpango wa RUJAT wa kuwajengea uwezo wanachama wake kupitia mafunzo na mikakati mbalimbali utasaidia kujenga msingi imara wa uandishi wa habari za vijijini unaozingatia weledi, ubunifu na matokeo chanya kwa jamii.

Alisema juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa habari ili kuhakikisha changamoto na mafanikio ya wananchi wa vijijini vinapata nafasi katika vyombo vya habari.

















Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top