Mwenyekiti wa mtaa wa Veta Musoma akemea tabia ya wazazi kuruhusu watoto kwenda vibanda vya kuchomea Filamu(Movie)

0



Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Veta kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma mkoa wa Mara Goodlack Nywamero, amewataka wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wao na kuwazuia kwenda katika vibanda vya kuchomea filamu(Movie), akieleza kuwa baadhi ya filamu zinazoonyeshwa katika maeneo hayo zina maudhui yasiyofaa kwa umri wao.

Amesema kuwa watoto wanaotembelea vibanda hivyo wanakutana na baadhi ya picha na maudhui yasiyozingatia maadili kwa watoto, hali ambayo kwa mtazamo wake inachangia mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watoto na vijana katika jamii.

Akizungumza katika kikao cha cha wazazi na uongozi wa shule ya msingi Mwisenge katika kujadili maswala ya taaluma na ushiriki wa wazazi katika malezi ya wanafunzi ili kupandisha kiwango wa ufaulu katika shule hiyo, amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuchukua jukumu la kuhakikisha watoto wao hawatumii muda mwingi kutazama filamu hizo badala ya kujikita katika masomo na shughuli nyingine za kujenga maendeleo yao.

Ameeleza pia kuwa, matumizi ya muda mwingi katika kutazama filamu yanaweza kuathiri mwenendo wa masomo na kuchangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi, kutokana na baadhi yao kutumia muda ambao wangepaswa kufanya maandalizi ya masomo katika kutazama filamu.

Katika hatua nyingine amesema katika mtaa wake amekuwa akichukua hatua za kuwafukuza watoto wanaokutwa katika vibanda hivyo ili kuwalinda dhidi ya maudhui yasiyofaa,.

Hata hivyo, amesema jitihada hizo zinakabiliwa na changamoto kutokana na baadhi ya wazazi wenyewe kwenda na watoto wao katika vibanda hivyo, jambo analodai linadhoofisha juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya maudhui yasiyofaa.

Kutokana na hali hiyo,Mwenyekiti huyo amewataka wazazi na walezi kushirikiana na viongozi wa maeneo yao katika kusimamia malezi ya watoto na kuwataka wafanyabiashara ya kuchoma fimamu(Movie) kuacha kuwaruhusu  watoto wadogo kukaa katika vibanda vyao, hukuakisisitiza pia jukumu la kujenga maadili na kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kukua halipaswi kuachiwa viongozi pekee bali linahitaji ushiriki wa familia na jamii nzima.

Esther Marwa ni mama wa watoto wawili na mkazi wa mtaa wa Mwisenge Pwani, anasema sio jambo jema wazazi kuwa ruhusu watoto kwenda kwenye vibanda vya kuchomea movie na kuwaacha watoto kuchoma movie wanazotaka kwa sababu hali hiyo inachangia watoto kuharibika hivyo wazazi wanapaswa kuchukua hatua haraka.

Kwa upande wake Faresi Mkama ambaye pia ni mkazi wa Mwisenge, ametoa wito kwa serikali kuangalia namna ya kudhibiti urushaji wa tamthilia kwenye televisheni kwa madai uwepo wa mfululizo wa tamthilia hizo kwenye chaneli za televisheni pia unachangia kiasi kikubwa watoto kushinda wanaangalia na hivyo kushindwa kujikita kwenye masomo na kufanya kazi za nyumbani.

Imeandikwa na Emmanuel Chibasa

📷Picha na AI

 

 

  

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top