Tanzania Yawakaribisha Wawekezaji wa Uturuki Kukuza Viwanda

0


Serikali imewakaribisha wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza nchini katika sekta za viwanda, teknolojia na uchakataji wa mazao ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ajira, kukuza biashara na kuimarisha uchumi wa Tanzania na Uturuki.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis L. Londo (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda ya Uturuki (MÜSİAD), jijini Dar es Salaam, Oktoba 16, 2026.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Londo ameipongeza MÜSİAD kwa kuitambua Tanzania kama kitovu cha uwekezaji na biashara katika Afrika Mashariki na Kati. Amewahimiza wanachama wa jumuiya hiyo kuelekeza mitaji yao katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, nguo, teknolojia na miundombinu ya uzalishaji.

Amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuboresha sera na sheria ili kujenga mazingira wezeshi na salama kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Tunawakaribisha wanachama wa MÜSİAD kuwekeza Tanzania kwa ubia au kwa kujitegemea. Soko letu halishii Tanzania pekee, bali linaunganisha fursa katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” amesema Mhe. Londo.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa MÜSİAD amesema Tanzania inavutia wawekezaji kutokana na nafasi yake ya kijiografia na utulivu wa kisiasa. Ameeleza kuwa jumuiya hiyo, yenye mtandao mpana wa kampuni, iko tayari kuleta mitaji na teknolojia ya kisasa itakayochangia maendeleo ya viwanda nchini.

Ili kutekeleza azma hiyo, pande hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano na taasisi za Serikali, ikiwemo Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), kwa lengo la kurahisisha taratibu za uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kuanzishwa na wanachama wa MÜSİAD.

Wakati huohuo, Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki umepongeza utayari wa Jumuiya hiyo kuwekeza nchini na kueleza kuwa utaendelea kuratibu juhudi hizo ili kusaidia kufanikisha uwekezaji unaotarajiwa.





Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top