DC Sima Awataka Wanafunzi na Wahitimu Kaizirege na Kemobos Kuepuka Wapotoshaji, Kulinda Amani ya Taifa Letu

0


Na Angela Sebastian 

Bukoba:  MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amewataka wanafunzi na wahitimu wa darasa la saba na kidato cha nne katika shule za Kaizirege na Kemebos kujiepusha na walaghai, wapotoshaji na watu wanaoweza kuvuruga amani ya nchi huku akisisitiza umuhimu wa kuwakataa watu hao kwa maslahi ya Taifa. 

Sima ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya wahitimu wa shule hizo yaliyofanyika hivi karibuni, akiwahimiza vijana kuwa wazalendo na kutambua wajibu wao katika kulinda amani na mshikamano wa Watanzania.

Akizungumza katika mahafali hayo, Sima amesema Tanzania haina mbadala, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuilinda na kuiombea ili iendelee kuwa mfano wa kuigwa duniani katika kudumisha amani na umoja.

 Amesema amani iliyopo nchini ndiyo inayowezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo kwa uhuru, ikiwemo kushiriki sherehe za mahafali katika mazingira ya utulivu.

“Hatuna Tanzania nyingine tofauti na hii tuliyonayo leo. Tumekuja katika mahafali haya, tumekaa, tunafurahi na kutulia kwa sababu tuna amani hii waliyoipigania waasisi wetu hivyo, amani isingekuwepo, hizi shamrashamra zisingekuwepo; tungegawa vyeti kimyakimya na kuondoka,” amesema Sima,

Audha  aliwataka wananchi kuendelea kuiombea nchi ili idumishe utulivu na kuimarisha maendeleo ambapo pia mkuu huyo wa wilaya amewahimiza wanafunzi kutumia maarifa na mbinu walizofundishwa na walimu wao katika kujibu mitihani ya Taifa kwa ufanisi, akieleza kuwa wanapaswa kuendeleza rekodi nzuri ya matokeo ambayo shule hizo zimekuwa zikifanya kwa zaidi ya miaka 19. 

Pia amesisitiza umuhimu wa kutangaza mafanikio ya Tanzania na kuunga mkono juhudi za uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, akitolea mfano mchango wa mkurugenzi wa shule hizo, Euston Ntagalinda.

Kwa upande wake, mkuu wa shule za Kaizirege na Kemiboss, mwalimu Kishe Ilamulila, amesema mafanikio ya shule hizo katika mitihani ya Taifa, mitihani ya majaribio (Mock) na mitihani ya kawaida yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya wazazi, walezi na walimu ambapo meongeza kuwa juhudi za walimu na wanafunzi, pamoja na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia yaliyowekwa na uongozi wa shule hizo kwa kushirikiana na Serikali, yameendelea kuchangia matokeo mazuri ya kitaaluma.

Taarifa iliyotolewa katika mahafali hayo imeeleza kuwa jumla ya wanafunzi 303 wa kidato cha nne wanaendelea na mitihani yao ya Taifa, huku zaidi ya wanafunzi 92 wakihitimu darasa la saba mwaka huu 







Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top