Nsekela Ampongeza Rais Samia kwa Kuendeleza Tunu za Mwenge wa Uhuru

0


 Na Angela Sebastian

 Kyerwa : Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Khalid Nsekela, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuenzi nyayo za waasisi wa Taifa letu kwa kuendeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru, unaoendelea kuwa chachu ya kuimarisha amani, uzalendo na upendo miongoni mwa Watanzania.

Amesema misingi hiyo imeendelea kuwa tunu muhimu inayolifanya Taifa kujivunia umoja na mshikamano wake.

Nsekela alitoa pongezi hizo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, baada ya kupata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Kyerwa wakati wa uzinduzi wa jengo la Wodi ya Wazazi katika Zahanati ya Kata ya Rukulaijo mbapo, jengo hilo limejengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kwa kutumia mapato ya ndani, likiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 386.1.

Kwa mujibu wa Nsekela, Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeendelea kupeleka fedha nyingi katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na afya, elimu, ujenzi wa barabara pamoja na kuanzisha na kuimarisha miradi inayowawezesha wananchi kiuchumi.

“Zahanati hii itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto, na kuondoa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita tano kufuata huduma hiyo katika Zahanati ya Nkwenda,” alisema Nsekela, 

Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, aliishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kuongeza huduma za afya katika zahanati hiyo kwa kuanzisha kituo cha kufanya upasuaji. 

Alisema hatua hiyo ni muhimu kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hiyo na itaendana na azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya karibu na maeneo wanayoishi.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zilipofika Wilaya ya Kyerwa, zilitembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.9. Miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi pamoja na kuongeza fursa za maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo.








Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top