Na Angela Sebastian
Wazee wa kimila maarufu kama Abenkorogo katika Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, wamepamba mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa kujitokeza kwa wingi huku wakiwa wamevalia mavazi yao ya asili.
Wazee hao walionekana wakiwa wamevaa kanzu nyeupe, koti,fimbo na kofia huku baadhi yao wakibeba vibuyu mikononi walishiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika katika Kijiji cha Gera, wakati wa makabidhiano ya mwenge huo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Hamis Maiga, na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Siima.
Katika tukio hilo, wazee hao pia walipewa fursa ya kuubeba Mwenge wa Uhuru ambapo kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wazo Mwang’onda, amesema amefurahishwa na namna wazee hao wa kimila walivyoshiriki katika tukio hilo muhimu lenye Tunu ya Taifa, akiwataka kuendelea kuwa mabalozi wa amani, mshikamano na maadili mema kwa vijana wao.
Mwang’onda amewataka wazee hao kuendelea kudumisha mila na tamaduni zao, pamoja na kuhakikisha zinahifadhiwa na kurasimishwa kwa ajili ya vizazi vijavyo ambapo itasaidia vijana kujifunza na kuthamini urithi wao wa kitamaduni.
Amesema ushiriki wa wazee wa kimila katika matukio ya kitaifa kama mapokezi ya Mwenge wa Uhuru una umuhimu mkubwa katika kuunganisha mila, utamaduni na uzalendo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha amani, umoja,malezi kwa vijana na mshikamano katika jamii .
Ukiwa katika Halmashauri ya Missenyi mwenge umezindua,kutembelea,kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba yenye thamani ya shl.bilioni 5.








