Wadau
kutoka sekta mbalimbali nchini Tanzania wamekutana mtandaoni kujadili namna ya
kuimarisha ushirikiano katika kujenga amani na mshikamano katika jamii kwa
kuzingatia tamko la “Declaration of Peace and Cessation of War (DPCW).”
Kikao
hicho cha Tanzania Peace Implementation Committee for the Realization of the
SDGs kilichoandaliwa na Heavenly Culture, World Peace, Restoration of Light
(HWPL), kilifanyika Agosti 15, 2026 na kuwakutanisha wadau kutoka sekta za
sheria za kimataifa, dini, elimu ya amani, vijana, vyombo vya habari na asasi
za kiraia.
Joseph
Kayinga ni mwandishi wa habari akizungumza katikakikso hicho amesema amani ni msingi wa jamii yenye maelewano na ametoa wito kwa waandishi
wa habari kutumia nafasi yao kama jicho na sauti ya jamii katika kuendeleza
ajenda ya amani huku pia amesisitiza umuhimu wa elimu ya amani kuingizwa katika
mitaala ya shule na vyuo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Mapunjo Forum George Cleopa Mapunjo, amesema amani
inaweza kuanzia katika familia na kuenea hadi kwenye jamii, taifa na dunia.
Amesema amani ya kweli haiwezi kupatikana bila haki na ulinzi wa haki za
msingi, huku akieleza dhamira ya kuendelea kushirikiana katika juhudi za
kujenga amani kwa kuzingatia misingi ya Ujamaa na kujitegemea.
Naye Zakie
Philimon Chatanda kutoka Upendo Media, amesema ushiriki
wake katika shughuli mbalimbali za HWPL umemsaidia kuona namna ujumbe wa amani
unavyoweza kuwasilishwa na kuenezwa katika jamii na hata kuvuka mipaka ya nchi.
Alieleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kupanuka hadi katika nchi nyingine kwa
lengo la kuchangia ujenzi wa amani katika jamii duniani.
Kikao hicho pia kilihusisha
mawasilisho kuhusu uzoefu wa ushirikiano, utangulizi wa madhumuni na misingi ya
DPCW, majadiliano ya vikundi na ufafanuzi wa nafasi ya Tanzania Peace
Implementation Committee. Washiriki walijadili hatua zinazoweza kuchukuliwa
katika jamii ili kuimarisha mshikamano wa kijamii, kujenga mfumo endelevu wa
ushirikiano wa amani na kuunganisha juhudi za amani kutoka sekta mbalimbali.








