MOROGORO: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewataka watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutenda haki na kuhakikisha wanakuwa na ushahidi madhubuti ili taasisi hiyo iweze kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan katika kesi inazozifikisha mahakamani.
Kauli hiyo ameitoa Jumatatu, Agosti 25, 2026, katika kikao cha mpango kazi cha watumishi wa TAKUKURU kilichofanyika mkoani Morogoro.
Waziri Kikwete amesema baadhi ya kesi zinazofikishwa mahakamani na TAKUKURU kutofanikiwa si kwa sababu taasisi hiyo inaonewa, bali kuna wakati maofisa wake hawajipangi vizuri katika uandaaji na uwasilishaji wa ushahidi.
Aidha, amewataka maofisa wa uchunguzi kujiridhisha na ushahidi wanaokusanya na kusimamia vizuri majukumu yao bila kuwakomoa watu, akisema si sahihi mtu kufikishwa mahakamani na kuendesha kesi kwa miezi mitano au sita, kisha mwishowe akashinda kesi kutokana na mapungufu katika ushahidi.
“Kinachofanya hatufanikiwi si kwamba tunaonewa. Kuna sehemu katika ushahidi wetu hatujajipanga vizuri, ama tumejipanga vizuri lakini tuna vitu katika kuunganisha ili mpaka mtu afungwe. Wakati mwingine lazima zile doti ziungane,” amesema Waziri Kikwete.
Amesema hali hiyo inampa sura isiyokuwa nzuri kama Waziri anayesimamia masuala ya utawala bora, kwa kuwa inaweza kuonekana kuwa baadhi ya maofisa wanatumika kuwapotezea watu muda wao badala ya kuhakikisha haki inatendeka.
“Kwangu mimi, nikiwa Waziri ninayesimamia utawala bora, hili halinipi sura nzuri. Linaonyesha kwa namna nyingine baadhi ya maofisa wanatumika kupotezea watu muda wao. Nchi inahitaji kujengwa,” amesema.
Waziri Kikwete amesema TAKUKURU ni taasisi yenye jukumu la kushughulikia makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, hivyo ni muhimu kwa maofisa wake kujiridhisha kuhusu ushahidi walionao pamoja na utayari wa kuwasilisha kesi mahakamani kabla ya kuwafikisha watuhumiwa katika vyombo vya sheria.
Amesisitiza kuwa maofisa wa TAKUKURU wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia haki ili kulinda heshima ya taasisi hiyo na kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi.









