DAR ES SALAAM: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, amempongeza Mheshimiwa Deo Ndejembi kwa kuanza rasmi majukumu yake mapya na kumuahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali kutimiza ahadi zake kwa Watanzania.
Akizungumza katika ujumbe wake wa pongezi, Waziri Kikwete amesema anatoa salamu za pongezi na dua njema kwa Mheshimiwa Ndejembi katika siku hiyo muhimu ya kuanza jukumu kubwa la kulitumikia Taifa.
“Salamu nyingi za pongezi na dua njema kutoka kwangu binafsi na Menejimenti nzima ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, kuja kwako Mheshimiwa Deo Ndejembi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika siku hii muhimu unapoapa kuanza kazi kubwa ya kuisaidia nchi yako na kumsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza ahadi zake za Ilani kwa Watanzania,” amesema Waziri Kikwete.
Amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Makamu wa Rais katika kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa maslahi mapana ya Taifa.
Waziri Kikwete amesisitiza kuwa msingi wa ushirikiano huo utakuwa ni kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma katika kutekeleza majukumu ya Serikali.
“Ahadi yetu ni ushirikiano mkubwa na kuchapa kazi kwa kiwango kikubwa sana,” amesema Waziri Kikwete.
Ameongeza kuwa uteuzi na kuapishwa kwa viongozi katika nafasi za juu za Serikali ni dhamana kubwa inayohitaji uzalendo, uadilifu na kujituma, huku akimtakia Mheshimiwa Ndejembi hekima, afya njema na mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.
Amesema dhamira ya viongozi wote wa Serikali inapaswa kuwa moja, kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwa wananchi kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi zinatekelezwa na kuleta matokeo chanya katika maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Ndejembi ameanza rasmi majukumu yake mapya baada ya kuapishwa, huku akitarajiwa kushirikiana kwa karibu na Rais na Serikali katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya kitaifa aliyopewa


